Wednesday, June 19, 2013
On 2:53 PM by Shambani Solutions No comments
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI
WA JAMII
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa
kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa nchini. Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu
waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara
yetu iliyopo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Dar es
salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo tarehe Juni 12,
2013. Utafiti huu uliongozwa na jopo la wataalamu kutoka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ikishirikisha program ya mafunzo ya Epidemiolojia yaani “Field Epidemiology and Laboratory Training
Program” pamoja na manispaa ya Ilala.
Hadi sasa idadi
ya wagonjwa ambao waliogundulika kuwa na dalili za ugonjwa huu ni 20 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza
maisha.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni
ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa
huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa
kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati
mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza
kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati
wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria
ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa
kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina
ya “Aedes”. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye
maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi
vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu
kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya
kuuma wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka
binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Homa
ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa
matibabu ya haraka. Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa
kutokana na dalili zitakazoambatana na
ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa
atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na
ugonjwa wa homa ya dengue
o Kuangamiza
mazalio ya mbu
ü Fukia madimbwi ya maji
yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi
vya mbu kwenye madimbwi hayo
ü Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka
mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari
yaliyotupwa hovyo, nk.
ü Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi
ya watu
ü Hakikisha maua yandayopandwa kwenye
makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
ü Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
ü Safisha gata za paa la nyumba ili
kutoruhusu maji kutuama
o
Kujikinga
na kuumwa na mbu
ü Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito
repellants”
ü Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na
mbu
ü Tumia vyandarua vyenye viuatilifu
(hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
ü Weka nyavu kwenye madirisha na milango
ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
·
Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu
wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na
Wakurugenzi.
·
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa
Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha uchunguzi
wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na
ongezeko la wagonjwa wenye homa.
·
Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya
mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa
atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze
kuchukuliwa.
·
Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya
maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa
atapatikana.
·
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa
huu katika hospitali 15 za mkoa wa Dar es salaam. Hospitali hizo ni pamoja na
hospital ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote 3 za manispaa ya Dar es salaam,
kituo cha afya Kigamboni, Kituo cha afya cha Mbagala Rangi tatu, Dispensari ya
Yombo Vituka, Kituo cha afya cha Mnazi mmoja, Dispensari ya Tabata A, Kituo cha
afya cha Bochi, Kituo cha afya cha Mbweni, Hospital ya Mission Mikocheni,
Hospitali ya TMJ, Hospital ya Regency na Hospital ya Hindu Mandal
·
Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza
kuthibitisha ugonjwa huu
·
Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa
tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na
hofu kuhusu ugonjwa huu.
Ugonjwa huu si mpya. Mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu
nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar
es salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40 na
hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.
Wananchi mnashauriwa kwenda katika
vituo vya tiba mara mnapoona dalili za ugonjwa huu.
Wizara inasisitiza kuwa hakuna
vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka
nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia
na kudhibiti ugonjwa huu.
Nsachris Mwamwaja
Msemaji
14 Juni 2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment