Tuesday, September 10, 2013

On 1:58 AM by Shambani Solutions   No comments


KATIKA kilimo ili uweze kupiga hatua ni lazima mazingira ya kufanyia kilimo yaboreshwe. Hiyo itasababisha wakulima wadogo na wale wasiojihusisha na kilimo wavutiwe sekta hiyo hivyo kufanya kazi hiyo.Katika mazingira ya nchi yetu, wakulima wadogo ndio wadau wakubwa wa kilimo na ndio wanaokabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuliko wakulima wakubwa.

Mfumuko wa bei unashuka na unahusika kwa asilimia kubwa kwenye bei ya mazao ya chakula lakini cha kusikitisha si kwamba uzalishaji wa mazao kwa wakulima umeongezeka bali ni kwa kuruhusu uingizwaji wa bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi inasikitisha.

Wakulima wa mpunga wilayani Kilombero, Morogoro wakizungumza kwenye mkutano wa wadau wa kilimo hicho wanalalamikia changamoto zinazowakabili likiwamo tatizo la maghala kupewa wawekezaji wa nje.

Mkutano huo ulioandaliwa na Jukwaa la Asasi za Kilimo (ANSAF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo Mjini na Vijijini (RUDI), ulihudhuriwa na wakulima wengi.

Mkulima Stanford Masige anasema ghala la Mbasa ambalo lipo Kijiji cha Mbasa limetolewa kwa mwekezaji wa nje ambaye ni Mchina na kuwaacha wakulima wa kijiji hicho wakiwa hawana mahala pa kuhifadhia mazao.

Ghala jingeni ni lile la Kikwawila, ambalo linatumiwa na mtu binafsi aliyefunga mashine ya kusaga unga badala ya kuhifadhi mazao, hivyo wananchi kulazimika kuuza mpunga ambao wamevuna kwa bei rahisi kwa kukosa sehemu ya kuhifadhia.
Lakini pia anasema serikali za vijiji zinaweka kodi kubwa na kusababisha vikundi vya wakulima kushindwa kumudu, hivyo kusababisha maghala hayo kupewa watu binafsi wanaobadili matumizi ya maghala hayo.

Kinachosikitisha ni kuwa maghala yaliyopo hayawatoshelezi wakulima, lakini hayo machache yaliyopo bado kumekuwapo na urasimu mkubwa hususan kwenye viongozi wa ngazi za vijiji ambao wamekuwa wakikodisha maghala haya kwa kujiamulia wenyewe.
Maghala mengi yaliyopo ni yale yaliyokuwa yanamilikiwa na vyama vya ushirika, vikundi mbalimbali pamoja na serikali za vijiji ambapo baadhi ya vyama vya ushirika vimekufa, hivyo maghala kusimamiwa na vijiji.

Mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima hususan wakulima wadogo na wakati kuwezesha mkulima kupata mikopo kwa urahisi chini ya mfumo wa vikundi, ushirika au kampuni kwa kutumia mazao kama dhamana.
Mfumo huo wa stakabadhi za maghala unatumika chini ya sheria Na. 10 ya 2005 na kutekelezwa na Kanuni za Mfumo za mwaka 2006.

Anasema kuendelea kuzorota kwa mfumo huu kunamrudisha nyuma mkulima na kusema mfumo huo umekuwa msaada mkubwa kwa kulinda ubora wa mazao na ushindani wa soko la ndani.Mfano mzuri sasa hivi kuna tatizo la kushuka kwa bei ya mpunga kutoka sh 100,000 hadi sh 50,000 kwa gunia la madebe kumi, hivyo mfumo wa stakabadhi ghalani ungekuwa unafanya kazi ipasavyo mkulima asingeweza kuumizwa kama hali ilivyo sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ansaf Audax Rukonge, anasema ili kuleta mapinduzi nchini katika sekta ya kilimo lazima serikali ibadilishe mtazamo na kuona kuwa kilimo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine. Anasema itafika wakati kama mkulima hatapata faida basi hataingia shambani, kwani mkulima amekuwa ni mtu wa kupata hasara kuanzia kwenye vocha za pembejeo hadi anapokuja kuvuna anawekewa ushuru mkubwa.

Rukonge anasema kuwa katika suala la maghala, mkulima angepaswa kupewa kipaumbele zaidi kuliko kuwapatia kipaumbe wawekezaji wa nje na kuwaacha wakulima mazao yao yakiharibika na kuuza kwa bei nafuu. Hata hiyo, katika hatua nyingine anasema wakulima wadogo wamekuwa na mchango mkubwa kwa taifa, kwani wao ndio wamekuwa wakizalisha chakula asilimia 80 ya chakula kinachozalishwa nchini.

Changamoto nyingine ambayo wakulima wa Kilombero wanalalamikia ni ushuru mkubwa unaotozwa na halmashauri, ambapo awali ulikuwa ukitozwa sh sh 1,000 kwa gunia la kilo 100 za mpunga lakini kwa sasa ni sh 5,000 kwa gunia lenye uzito huo.
Mkulima, Masumbuko Fransis, anasema kuwa wanakumbana na ushuru kwa zaidi ya mara tatu ambapo tayari walikwisha kuandamana na kupigwa mabomu, lakini bado halmashauri inaendelea kutoza ushuru huo. “Wanunuzi wananunua kwenye wilaya nyingine ambazo zina ushuru mdogo, lakini pia kushusha bei ya mpunga kwa kuwa wametozwa ushuru mkubwa na serikali ambapo mkulima ndiye anayeumia,” anasema.

Anasema watumishi wa serikali na madiwani waliochaguliwa na wananchi ambao ni wakulima wanashindwa kuwatetea wananchi na kuwaacha wakikandamizwa na ushuru mkubwa ambao wanatozwa.
Mwekahazina wa Halmashauri ya Kilombero, Mbwana Msangi, ambaye alitakiwa kujibu maswali ya wakulima na Kaimu Mkurugenzi aliyefika kwenye mkutano kwa nyakati tofauti wanasema licha ya ushuru kuwa mkubwa lakini wanalazimika kufanya hivyo, kwa kuwa halmashauri inajiendesha kwa kutumia ushuru wa mazao kwa asilimia kubwa.

Wadau na wakulima waliofika kwenye mkutano huo walipendekeza kushirikishwa kwa wakulima katika suala la ushuru. Ifike wakati serikali iwe sikivu juu ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wakulima ili na wao kuweza kufanya kilimo cha biashara na kujikwamua kimaisha na si wakulima walime wao lakini wanufaike wafanyabiashara.

Source; http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=53734

0 comments:

Post a Comment