Sunday, September 8, 2013

On 7:26 AM by Shambani Solutions   1 comment
Simon Kinabo akionyesha bwawa lake la samaki
Mawazo ya wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini katika miaka ya karibuni  imekuwa ni namna ya kupata  ajira zenye tija.Ndoto ya wengi ni kupata kazi za kipato kizuri nambazo zitawawezesha kuishi vizuri, kumiliki gari, kujenga nyumba na mambo mengine lukuki.Hata hivyo, baadhi wamekumbana na tatizo la ajira ambalo limewasukuma katika kubuni miradi ambayo  itawawezesha kumudu maisha na changamoto zake.

Mmoja wao, Simon Kinabo, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichoko Morogoro ameamua kujiajiri baada ya  kubuni mradi wa  ufugaji wa samaki.Mradi huo  unaoitwa Rombo Unique Aquaculture, upo kilomita 60 kutoka mjini Moshi na kilomita nne kutoka makao makuu ya Wilaya ya Rombo, eneo la Mkuu. Anasema akiwa mwanafunzi katika chuo hicho, akisomea Shahada ya Sayansi ya Viumbe wa Majini (BSc Aquaculture) alihamasika na somo la uzalishaji wa samaki na ndipo akaamua kuanzisha mradi huo kwa mtaji wake.“Katika fedha zile za mkopo,  kila nikipewa na Serikali, nilichukua kiasi kidogo na kuanzisha nyumbani mradi wa kufuga samaki. Niliamini ni mradi mzuri ambao unaweza kubadili maisha yangu,” anasema. Anaongeza kuwa alianzisha mradi huo  kwa kuchimba bwawa dogo na kuanza kuzalisha samaki, kwa lengo la kuja kuwauza baadaye.

Mkopo wa CRDB
Anasema akiwa mwaka wa pili SUA  alipata taarifa ya kuwapo mradi wa SUGECO unaoendeshwa na chuo hicho na CRDB ambao unalenga kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya juu kuingia katika ujasiriamali.
“Baada ya kupata taarifa hizo nilijitokeza kuandika andiko la kuomba fedha na baada ya usaili, andiko langu lilipitishwa na chuo na CRDB,” anasema. Anaongeza kuwa baada ya kupitishwa andiko lake, alipokea mkopo wa Sh20 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi.Baada ya kupokea fedha, aliamua kupanua bwawa  hilo na pia kuliongezea mifumo ya kuingiza maji kutoka Mto Ngwasi na kutoamaji ili liwe la kisasa. “Nilinunua mabomba 100 ya futi 2,000 na sasa bwawa langu lina urefu chini, mita  tatu hadi sita na upana mita 30,” anaeleza.Anasema kuwa baada ya upanuzi wa bwawa alinunua samaki wadogo 3,000 kutoka Gereza la Karanga mjini Moshi ambao walikuwa ni  wa jamii ya perege na kambare. Anaongeza kuwa  kila kifaranga cha samaki alikinunua kwa Sh300 na kwamba hiyo ilikuwa Mei 5, mwaka  jana, alipoanza kuwapandikiza bwawani mwake.
Mafanikio ya mradi
Hadi sasa, Kinabo anasema bwawa lake linao  zaidi ya samaki  40,000, kati ya hao wakubwa ni 10,000 na wadogo 30,000. Anasema , Juni mwaka huu  anatarajia kuanza kuvua samaki na  matarajio yake  ni kuvua tani  nne  za samaki. “Nina imani tani hizo nne, nikivua naweza kupata zaidi ya Sh60 milioni na tayari nimepata masoko,” anasema  msomi huyo.Anasema tayari, amefanya mazungumzo na wakuu wa shule kadhaa za sekondari  wilayani Rombo, Hospitali ya wilaya hiyo na maeneo kadhaa ambao wamekubali kununua samaki wake.Kwa kutambua kuwa hawezi kufanya kazi  hizo peke yake, mjasiriamali huyo msomi amemwajiri mtunza mazingira, James Edmund,  pia hivi karibuni atakuwa na walinzi wawili na muuzaji wa samaki.

Kiwanda cha kusindika samaki
Lengo lake la baadaye ni kuanzisha kiwanda cha kusindika samaki, ingawa awamu ya kwanza itakuwa ni kuuza samaki. “Najua baada ya mauzo na kurejesha mkopo, nitabaki na fedha kidogo ambazo nitazitumia kununua mashine ndogo na vifaa vingine vya kiwanda cha kusindika samaki,” anasema.Kwa taaluma alizonazo, Kinabo anaeleza kuwa haoni ugumu wa kuwa na kiwanda kwani baada ya miaka mitano, atakuwa na samaki wengi katika mabwawa yake ambao haiwezekani wote kuuzwa wakiwa ghafi. “Hili la kiwanda halikwepeki kwani mradi wangu, faida kubwa itapatikana  kwa kuwa na kiwanda ambako nitaweza kuuza samaki waliosindikwa na kuandaliwa vizuri, ”anasema.

Changamoto
Mradi  huo  kama ilivyo miradi mingine, una changamoto nyingi ambazo tayari amepitia. Anasema baada ya kuanzisha mradi huo, kuliibuka kikundi cha watu ambao walianza kupinga kwa maelezo kuwa atamaliza maji kijijini Kuini. Hata hivyo, anasema maji hayo, yanapita katika kijiji hicho yakitokea katika Mto Ngwasi.
Anaeleza kuwa baadhi ya wanakikundi walifikia hatua ya kumhujumu kwa kumwekea sumu  bwawani ambapo idadi kubwa ya samaki walikufa. Hata hivyo, anasema baada ya hali hiyo, aliamua kuanza kutoa elimu ya mradi huo na kwa sasa watu wengi wanamuunga mkono.“Niliona kupingwa kwa mradi ni changamoto na samaki walivyouliwa pia ni changamoto, sikwenda polisi kulalamika bali niliamua kutoa elimu kwa majirani na wanaopinga na namshukuru Mungu sasa tunakwenda vizuri,” anasema. Wito wake kwa wahitimu wa vyuo vikuu  ni kwamba, hivi  sasa soko la ajira lina ushindani mkubwa, pia kwa kiasi kikubwa halikidhi mahitaji ya wahitimu walio wengi.Kwa hiyo, mojawapo ya njia za wahitimu kujikomboa ni kutumia elimu yao, kubuni miradi kwani karibu kila taaluma ina nafasi kubwa ya kubadili maisha ya  mhitimu kuliko kukimbilia kutafuta ajira. “Wasomi tuache kukimbilia kazi za kuajiriwa kwani tunaweza kutumia elimu yetu kujiajiri na kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo,” anaasa.
Maisha yake
Kimaisha, yeye ni mzaliwa wa Rombo, Kilimanjaro. Alisoma  Shule ya Msingi Mharu, Rombo kati ya 1992-1998 na baada ya hapo alijiunga na Shule ya Sekondari ya Horombo mwaka 1999 - 2002. Masomo ya kidato cha tano na sita aliyapata katika Shule ya  Sekondari  Majengo mjini Moshi  kabla ya  kujiunga na SUA.

Kauli ya CRDB
Dorah Ngaliga  ambaye ni Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu wa CRDB, anasema mradi wa  Kinabo ni miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na benki hiyo, ambayo inafanya vizuri.Anasema  benki hiyo hadi sasa imetoa Sh300 milioni kwenye miradi ya kuwasaidia wahitimu wa vyuo vikuu nchini  kuingia katika ujasiriamali.“Tuna imani kubwa na hawa vijana ambao wamekuwa wakileta maandiko ya miradi na hadi sasa zaidi ya 300, wamejiajiri katika miradi hii na lengo letu sisi ni kuhakikisha wahitimu wa vyuo wanajiajiri wenyewena siyo kutegemea ajira,” anasema Ngaliga.Anaongeza kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa dhamana ya cheti, kwa mhitimu wa chuo kikuu na hadi sasa miradi karibu yote ambayo imewezeshwa na benki inakwenda vizuri.

Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari+ya+ndani/-/1724700/1761352/-/item/0/-/482iw1z/-/index.html

1 comment: