Tuesday, September 10, 2013

On 2:17 AM by Shambani Solutions   No comments
“SISI tumeamua kuwekeza katika sekta ya elimu na kilimo hasa Ruvuma kutokana na historia ya mkoa huu.” Hayo ni maneno ya Meneja Mkuu wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB), Shedehwa Optati, anayoyasema wakati akifanya mahojiano na Tanzania Daima. Akizungumzia historia, mafanikio na mchango wa benki hiyo kwa wananchi anasema MCB ilianzishwa miaka kumi iliyopita baada ya kuanguka kwa Shirika la Maendeleo Mbinga lililojulikana kama MBICU. “Kuanguka kwa MBICU kulileta mbinu mpya kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya ya Mbinga na huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuanzishwa kwa MCB; Julai 30, mwaka 2003 kwa mtaji wa sh milioni 153,” anasema.

Shedehwa anasema MCB ilipoanzishwa iliwalenga watu wa hali ya chini kuliko matajiri ambao ni vigumu kushawishika kuweka pesa kwenye benki zenye mitaji midogo hivyo, kuwateua wakuu ambao ni wakulima, wajasiriamali wadogo na watu wenye kipato cha kati. Anasema benki za wananchi zinalenga katika maeneo maalumu, hivyo ni uhakika kwa wananchi wa eneo husika kupata huduma za kibenki, ndiyo sababu wao kama MCB waliamua kutoa huduma katika Wilaya ya Mbinga sambamba na Mkoa wa Ruvuma. Shedehwa anasema benki yake kwa sasa inamilikiwa na wananchi ambao ni wawekezaji wa Ruvuma, wengi wakiwa wanatoka Mbinga. Pia anasema dira ya MCB ni kuwa asasi kiongozi ya kifedha itakayotoa huduma bora za kifedha kwa wananchi. Shedehwa alisema benki hiyo inawajali na kuwasikiliza wateja, kutoa huduma bora za kifedha, kutenda kazi kwa uwazi, kutunza siri za wateja na kuwajibika katika jamii hususan katika sekta ya elimu.

Pamoja na mambo mengine, Shedehwa anasema kuwa MCB inatoa huduma mbalimbali za kibenki, ikiwemo akaunti za akiba binafsi, akiba za vikundi, amana za muda maalumu, akaunti maalumu za asasi za kiserikali na akaunti za mwana. “MCB tuna huduma za mikopo kama vile mikopo ya biashara, mikopo ya kifuku kwa biashara za kati, hasa wakulima hususan katika kipindi cha mvua ambapo mkulima huwa na hali ngumu, mikopo ya uzalishaji mali na mikopo ya elimu,” anasema. MCB inashirikiana na Benki ya Posta katika huduma ya ‘Western Union’ kwa ajili ya kutuma na kupokea pesa duniani kote.

Anasema pia benki inashirikiana na wakala wa huduma ya kuweka na kutoa pesa ya M-Pesa na Tigo Pesa. Pamoja na huduma hizo zote pia benki imejiunga na mtandao wa ATM za Umoja Switch, zinazomuwezesha mteja kutoa pesa katika mikoa yote nchini. Akielezea mafanikio ya benki hiyo, anasema wameweza kuleta msisimko wa uchumi wilayani humo, Songea Vijijini na Mjini kutokana na na huduma za MCB kuwafikia zaidi ya wananchi 34,000 ambao hawajawahi kutumia huduma za kibenki hasa vijijini. “Pia imeweza kukuza zao la kahawa na ngano kwa kiasi kikubwa pamoja na mazao mengine kama vile mpunga, zao ambalo lilikuwa ni nadra na pia kuna vinu vya kukobolea zao hilo zaidi ya vitatu. “Hivyo tunajivunia kwa kiasi kikubwa kuwa washiriki wa kuinua kilimo wilayani humu,” anasema.

Anafafafua kuwa wameweza kufungua vituo vya huduma kwa wateja kumi vinavyotoa huduma za kibenki Ruvuma. “Pia tumeweza kutoa nafasi za ajira 46 ikilinganishwa na mwaka 2003 ambapo tulianza na watu sita, sambamba na mchango mkubwa tunaoutoa kila mwaka katika sekta ya elimu ili kuhakikisha Ruvuma inainuka kielimu na kuondoa ujinga,” anabainisha Shedehwa.

Shedehwa anasema wanachangia kiasi cha sh 300,000 kwa ajili ya shughuli za kijamii kama michezo na watoto wenye mahitaji maalumu ikiwamo yatima lakini wanatamani kutoa zaidi. Shedehwa anaeleza kuwa changamoto za kuendesha benki ni nyingi sana, likiwamo tatizo la mitaji. “Sisi MCB tunafadhiliwa na taasisi ya FSDT, Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia, Taasisi ya Bill Gates Foundation pamoja na Serikali Kuu kwa ajili ya mafunzo ya wajasiriamali na walinunua hisa za upendeleo 473 kwa ajili ya kuinua mtaji wetu, kwani ifikapo mwaka 2017 tunatakiwa tuwe tumefikia mtaji wa sh bilioni 2,” anasema.

Shedehwa anasema changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni ucheleweshaji wa urejeshaji wa mikopo kwa wateja wao, jambo ambalo lina wapunguzia mtaji na kurudisha nyuma utendaji kazi na ukuaji wa benki. 

Wito anaoutoa kwa wateja na wananchi wa Mbinga kwa ujumla ni kulipa mikopo yao kwa wakati sambamba na kuwashauri wawe watumiaji wazuri wa huduma ya M-Pesa na Tigo Pesa kwa kuwa ni njia rahisi na salama katika uhifadhi na upokeaji wa fedha popote. “Ninawahimiza wananchi wawe wanunuzi wa hisa kwa ajili ya kukuza mtaji na kuongeza umiliki katika benki, pia wanasiasa waache kupiga kelele bungeni juu ya riba kubwa ya asilimia 24 inayotolewa na benki katika mikopo, kwani gharama za uendeshaji ni kubwa na sisi wenyewe tunakopa pesa kutoka kwenye benki kubwa, hivyo ni lazima tufidie,” anafafanua.

Shedehwa anasema wataendelea kutoa mchango wao na kuelekeza nguvu zao katika sekta ya elimu na kilimo kwa wakazi wa Ruvuma.

SOURCE: http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=53733

0 comments:

Post a Comment