Wednesday, June 5, 2013

On 2:58 PM by Shambani Solutions   No comments




Waziri  mkuu wa Tanzania Mh Mizengo Pinda
 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakazi wa wilaya mpya ya Mlele mkoani Katavi walime mazao mbadala ya biashara kama alizeti, karanga na ufuta kwa sababu yanachukua muda mfupi na hivyo kuleta kipato cha haraka.Ametoa wito huo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nsenkwa mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye zahanati ya kijiji hicho akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.


Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kuachana na mazoea ya kulima tumbaku kwa vile inachukua muda mrefu hadi kukomaa na inachangia uharibifu kubwa wa mazingira kwani inahitaji kuni nyingi wakati wa kukausha. “Tumbaku hivi sasa haina bei kwa sababu wanaopanga bei ni wakubwa huko nje… tuangalie mazao ya alizeti, ufuta na karanga kwa sababu yanatoa pesa kwa haraka zaidi. Mfano mzuri ni Singida ambao wamekuja juu kiuchumi kwa sababu ya zao la alizeti,” alisisitiza.

Aliwataka wakazi hao waangalie ufugaji nyuki kama fursa ya kipekee kwa sababu mkoa huo umejaliwa kuwa na misitu mingi na unaweza kuongeza kipato cha mkoa wao. “Asali ni dawa, asali ni chakula, asali ni biashara na ina soko hapa nchini hadi nje ya nchi. Changamkieni fursa hii, ongezeni uzalishaji wa asali na nta,” aliongeza. Aliwashauri pia waangalie uwezekano wa kulima miembe ya kisasa kwa sababu inazaa kwa wingi na katika kipindi kifupi mno. “Hii miembe yenu inazaa maembe 10-20 kwa mwaka lakini ya kisasa inazaa hadi maembe 10,000, ikiwa chinichini tu,” alisema.

Akihimiza kanuni bora za kilimo, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Mlele aliwataka waachane na kilimo cha matuta na badala yake watumie kilimo cha sesa. “Ekari moja ya mahindi inapaswa ikupatie magunia 20-25 ya mahindi, sasa wewe unalima ekari tatu na kuvuna magunia 10, sababu kubwa ni nafasi zinazopotea kwenye miraba ya matuta, alisema.
“Ni lazima tuondokane na kilimo hiki kwa sababu hakina tija na tena kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika kupanda mazao,” alisisitiza.

0 comments:

Post a Comment