Saturday, June 22, 2013

On 8:23 AM by Shambani Solutions   No comments




Dar es Salaam. Wanasayansi nguli nchini wamesema wakulima wa Tanzania wanaweza kuwa matajiri kwa kugeuza kilimo chao, kuwa cha biashara iwapo wataelekezwa kikamilifu utumiaji teknolojia mpya za uzalishaji.

Walisema teknolojia hizo zina uwezo wa kumfanya mkulima azalishe mazao mengi eneo dogo kwa kumea vizuri kwa mvua kidogo, kuwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya wadudu na magonjwa ya mimea.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu juzi, Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Mimea ya Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk Roshan Abdallah alisema miongoni mwa teknolojia hizo ni bayoteknolojia.

Dk Roshan alikuwa Zanzibar ambako anajadili na wanasayansi wakiandaa mwongozo wa tathmini kabla ya kukubalika kwa matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni nchini.

“Kinachotakiwa ni wanasayansi kutumia uwezo wao kubuni mbinu mbalimbali zitakazowasaidia wakulima,” alisema.
Alisema wakati huu ambao wakulima wanakumbana na vikwazo vingi kama ukame, magonjwa na wadudu waharibifu wa mimea, ni muda mwafaka wa kuwapatiwa mbinu madhubuti zitakazowawezesha kuondokana na tatizo hilo.

Hata hivyo, Dk Roshan alionya wanasayansi kuwa lazima wahakikishe wanatekeleza kazi zao kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi zinazosimamia teknolojia za GMO.

Maelezo ya mtafiti huyo yamekuja siku chache baada ya mtaalamu mwingine wa Kilimo, Profesa Joseph Ndunguru wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Mikocheni kusema teknolojia ya bayoteknolojia inawezekana kutumika kikamilifu nchini.
Alisema anaamini bayoteknolojia ndiyo njia pekee iliyosalia kumkomboa mkulima wa Tanzania.

0 comments:

Post a Comment