Friday, June 14, 2013
On 3:04 PM by Shambani Solutions No comments
Ijumaa iliyopita itajulikana kama siku mlango mdogo ila muhimu sana
ulipofungua kitasa chake kwa baadhi ya wananchi wanaojituma kikazi na
kibiashara Tanzania. Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitembelea
soko la mboga na matunda lililoko Leytonstone, mashariki ya
London.Matembezi yalidhihirisha mahusiano ya ujirani mwema kati yetu
Watanzania na Kenya yenye kampuni iliyoshajijenga ndani ya soko hili
maarufu na kubwa sana.
Matunda yakiwa sokoni UK |
Soko hilo linaloitwa Spitalfields si sehemu inayofahamika na wengi
wanaoishi Uingereza licha ya kwamba jina hilo si rahisi kutamka au
kuandikwa. Lakini Spitalfields (tamka “Spitol-fildz”), itakua eneo
muhimu sana kwa vijana, wakulima na wafanyabiashara Tanzania, miaka
ijayo.
Waziri Mkuu akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi wa SACOMA, Sam Ochieng aliyeshika kiazi kikuu toka Ghana. |
Hapa ndipo mboga na matunda toka sehemu mbalimbali duniani huletwa
halafu zikasambazwa katika maduka makubwa ya vyakula Uingereza nzima.
Hivyo basi mlango kufunguliwa ni “uwanja muafaka” kwa wote wanaojituma
na kutaka maendeleo kiuchumi.
Spitalfields ina zaidi ya miaka mia tatu. Ingawa ilipoanzishwa makao
yake yalikuwa mtaa wa Brick Lane karibu na Liverpool Street, leo tawi
jipya, New Spitalfields Market limehamishwa karibu uwanja yalipofanyika
mashindano ya Olimpiki mwaka jana. Tawi hili lilifunguliwa rasmi 1991
na linaongoza Ulaya nzima kwa usambazaji wa matunda na mboga toka nchi
zenye joto duniani.
Kati ya nchi hizo ni ndugu zetu wa Kenya kupitia kampuni ya
SACOMA(“Sahara Communities Abroad”) iliyoanzishwa mwaka 2000 kuendeleza
wananchi wasiojiweza kiuchumi na kielimu walioko jimbo la kusini ya
jangwa la Sahara wanaozungumza Kiswahili. Licha ya kusafirisha bidhaa na
kuziuza New Spitalfields, SACOMA , anasema msemaji wake Bi Perez
Ochieng hutoa ajira kwa takriban watu 30,000 Ulaya na Kenya.
Meneja Mwendeshaji Masoko wa New Spitalfields Market, Nigel Shepherd akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu. Kando ni Juma Bozdogan wa SACOMA. |
Waziri Mkuu na Perez Ochieng wa SACOM |
Perez Ochieng, mumewe Sam Ochieng kupitia SACOMA na meneja mwendeshaji
New Spitalfields, Bw. Nigel Shepherd walimtembeza Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akiongozana na Balozi wetu Ungereza , Mhe Peter Kallaghe,
mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania, London, Yusufu Kashangwa na
maofisa wengine.
Ubalozi wa Tanzania Uingereza ndiyo ulioratibu na kuandaa tukio zima. Waziri Mkuu na wenzake walikuja London kuhudhuria mkutano wa
kimataifa unaoangalia namna ya kuondoa njaa na umuhimu wa lishe bora kwa
kina mama na watoto ulimwenguni. Mkutano umeandaliwa na asasi za
serikali na zisizo za kiserikali kukutanisha mataifa makubwa (yaani G8),
wachangiaji, wadhamini na watoaji misaada kwenye asasi hizi zenye
lengo la kutokomeza njaa na kusaidia kuwapatia kina mama na watoto lishe
bora.
Baada ya kutembelea maeneo ya ndani sasa pinda atembelea maeneo ya nje ya soko |
Baada ya matembezi ndani ya ghala mbalimbali, SACOMA iliandaa kikao
kifupi kuonyesha namna (na pia) mazao gani huuzwa. Baadhi ya mazao
yaliyowekwa mezani kilipofanyika kikao ni pamoja na mahindi ya
kuchemsha, ndizi kisukari, juisi za matunda, viazi vitamu, maembe
sindano na mboga maarufu ya Sukumawiki ambayo hutumiwa zaidi Kenya.
Sukuma Wiki iliyo ndani ya familia ya mboga za kabeji huuzwa tayari
imefungwa kwenye mifuko na SACOMA.
Picha ya pamoja. Waliokaa, Bw. Nigel Shepherd, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bi. Perez Ochieng, Balozi Peter Kallaghe. Waliosimama nyuma, Bw. Sam Ochieng (SACOMA), Bw. Hugh Morris (mwenyekiti wa kamati ya masoko London) na Bw. David Smith, CDE, (mkurugenzi wa masoko jiji la London). |
Wakati wa kikao hicho wazungumzaji wahusika walieleza namna ambavyo soko
litawafaidi wakulima , vijana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale
wanaojituma.
Meneja Mwangalizi wa soko, Nigel Shepherd na Wana SACOMA walifafanua
baadhi ya masharti yanayotakiwa kufikiwa kuleta bidhaa hizi sokoni.
Mojawapo ni kuzingatia taratibu za uuzaji wa mazao uliowekwa na Jumuiya
ya Nchi za Ulaya (EU). Taratibu hizo ni mathalan upandaji mazao
unavyofanywa kusudi umudu safari ya muda mrefu, hifadhi yake katika
makasha ya baridi, usafi wa jumla, ufungaji na utangazaji (branding).
Perez Ochieng alitoa mfano namna SACOMA ilivyojitahidi kuwahusisha
vijana wa Kenya katika kilimo ambacho kimewaletea ajira na kuboresha
maisha yao. Akifafanua Perez alisema kawaida vijana waishio mijini huwa
hawavutiwi na kazi za kilimo lakini kuna “mengi ya kuzingatiwa ikiwemo
kazi za kupakia bidhaa, kuzifunga katika mifuko, uendeshaji magari,
uandishi wa makasha, nk.
Waziri Mkuu , Mizengo Pinda akitoa shukrani zake na kuahidi uwezekano wa Tanzania kujitayarisha ipasavyo. |
Akiendeleza hoja zaidi Waziri Mkuu ambaye kazaliwa mazingira ya kilimo
alisema shughuli hii imedunishwa na mtazamo kuwa ni kazi ngumu na chafu
ya jembe tu. “Inabidi tuweke mazingira yatakayowafanya vijana waone
kazi zao zinaweza kupata soko. Kazi kubwa inahitajika kufanywa kuwafanya
vijana wapende kilimo.”
Akitoa mfano wa kampuni ndogo ya vijana wa Gongo Seke walioamua kufanya
biashara ya kilimo cha bustani aliyotembelea karibuni mkoa wa Mwanza,
Waziri Mkuu alisema hiyo inathibitisha wapo wanaoweza kufuata fani hii.
am Ochieng kashikilia boga huku Waziri Mkuu akimsikiliza. Kulia ni mwanahabari wa Uganda, Danny Lutaya. Nyuma yake Haruna Mbeyu wa CCM |
Mheshimiwa Pinda aliwahakikishia wenyeji kwamba si tatizo hata kidogo
kwa Tanzania kuuza bidhaa zake. Akithibitisha uzoefu wake kama mkulima,
Waziri Mkuu aliwachekesha wasikilizaji wake aliposhika moja ya ndizi
kisukari zilizokua mezani akasema Watanzania wanaweza kuleta ndizi
zilizovimba zaidi na maembe dodo makubwa kuliko yale sindano
yaliyoonyeshwa.
Waziri Mkuu akiwa ndani kabisa ya soko na wahusika wote. Kulia kwake ni diwani wa wilaya ya Barking, Elizabeth Kangedhe, mfanyakazi wa SACOMA, Juma Bozdogan. Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Perez Ochieng na Nigel Shepherd. Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe amesimama nyuma yao. |
Kufuatana na takwimu zilizotolewa na idara ya habari ya CNN mwaka jana,
ingawa uchumi wa Afrika unatazamiwa kukua kwa asilimia 4.5 idadi ya
vijana inatazamiwa kuongezeka mara mbili barani mwaka 2045. Leo asilimia
30 ya vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 29 hawana ajira katika
jamii nyingi za Afrika.
Source:http://kitoto.wordpress.com/2013/06/10/changamoto-uwezekano-wa-wakulima-vijana-na-wafanyabiashara-kuuza-bidhaa-uingereza/#more-1998
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment