Saturday, June 8, 2013
On 4:01 AM by Shambani Solutions No comments
Hivi karibuni Mkoa wa Simiyu ulishuhudia mkutano maalumu wa
watu mashuhuri wa mkoa huo, waliokusanyika kwa siku moja ili kutoa mwelekeo
mpya wa mafanikio ya kilimo cha pamba.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Katibu
Tawala, wakuu wa wilaya zote, viongozi wa Bodi ya Pamba, wakurugenzi wa
halmashauri, maofisa kilimo, wamiliki wa jineri za kuchambua pamba, kampuni za
kununua pamba, wakulima wa pamba na waalikwa kwa mila na desturi,
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kupitia vyombo vya habari, mkutano huo
pamoja na mengineyo, ulilenga kupanga mikakati ya kuboresha kilimo cha pamba
kwa mkataba.
Mkutano ulikubaliana kuimarisha kilimo cha mkataba, ambapo wamiliki wa
jineri, kampuni za kununua pamba zitaingia mkataba na wakulima wa pamba wa
kulima pamba itakayokuwa na uhakika wa soko.
Kampuni zitakubaliana na wakulima walime pamba ya ubora unaotakiwa, lakini
pia kampuni nazo zitatoa mikopo maalumu ili mkulima afanikishe kilimo hicho na
baadaye malipo yatakatwa wakati wa mauzo ya pamba.
Hii ina maana kwamba kampuni zinazoingia mkataba na wakulima, zitakuwa
karibu nao kwa kuangalia upandaji, palizi, uvunaji na utunzaji wa pamba kwamba
unazingatia ubora. Wakulima hawatatakiwa kuchanganya pamba na mchanga, ama
kuilowesha kwa nia ya kuongeza uzito.
Mpango huo ni mzuri kama kampuni nazo zitazingatia mkataba bila kuweka
visingizio vingine vya kutaka kuwaibia wakulima. Ipo haja kwa viongozi na
wakulima wa pamba wa Mikoa ya Geita, Shinyanga na Mwanza kutangaza mikakati ya
kuboresha kilimo cha pamba.
Kampuni hizo lazima ziwakopeshe wakulima wa pamba kwa riba isiyowaumiza,
zipange bei nzuri ya kununua pamba, zitoe misaada ya kibinadamu kwa wakulima
wakikumbwa na shida ya kijamii.
Kampuni zinazoingia mkataba ziwe na malengo ya kuongeza bei ya pamba kwa
kila mwaka na siyo kudumaza. Zishiriki katika kuboresha barabara za vijiji vya
wakulima, ujenzi wa zahanati na kusaidia sekta ya elimu.
Kwa hali hiyo, kilimo cha mkataba kitakuwa na tija kwa pande zote kwani
wakulima watahamasika zaidi na kuongeza maeneo ya kilimo cha pamba.
Utaratibu wa kampuni za biashara ama usindikaji wa mazao kuingia mkataba na
wakulima unaweza kuigwa pia na wanaohusika na mazao ya korosho hususan wa Mikoa
ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Wakulima wa korosho kwa sasa wako kwenye dimbwi la mawazo yasiyoisha. Katika
kutafuta moja ya suluhisho, viongozi wa Mkoa wa Lindi hivi karibuni walikaa
kikao na kutangaza kuifuta kampuni moja iliyokuwa ikinunua korosho kwa madai ya
kuchochea utata katika ununuzi wa zao hilo.
Pamoja na kwamba kampuni husika haikupewa nafasi ya kujitetea, lakini ukweli
ni kwamba wakulima wa korosho hadi sasa wanahitaji suluhisho la kudumu kwa
kuweka utaratibu wa kilimo cha kibiashara na mkataba.
Kwa mfano suala la kufufua viwanda vyote vya kubangua korosho lisimamiwe kwa
dhati na baada ya kufufuliwa, wamiliki wa viwanda waingine mikataba ya
makubaliano na wakulima wa korosho.
Matatizo ya wakulima ni mengi kwa mazao yote. Serikali inawajibika
kuwasaidia wakulima na kuwapa miongozo ya kuondokana na matatizo hayo.
Kwa mfano China imeonyesha nia ya kununua tumbaku nyingi ya Tanzania. Ipo
haja kwa Serikali kuwasaidia na kuwaeleza kwa uhakika wakulima wa tumbaku
mipango hiyo ili waweze kulima tumbaku inayokidhi soko la China.
Soko zuri la tumbaku huko China liwafikie wakulima siyo kuwanufaisha watu
wachache kupitia vyama vya ushirika na kampuni wanazoziunda wajanja kwa madai
ya kuwasaidia wakulima kupitia mikataba yao na China. Jamani wakulima
waheshimiwe na wapewe haki zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment