Friday, March 29, 2013
On 9:54 AM by Shambani Solutions No comments
Safari hii hajaja sokoni kuchukua fedha kwa njia haramu au ya
vitisho, lakini kulipwa kwa magunia matatu ya spinachi na sukuma wiki
aliyoyaleta alfajiri, ikiwa ni sehemu ya maisha yake mapya tofauti na makosa ya
vurugu.
Irungu alikuwa ni mmoja kati ya
majambazi walioogopwa sana katika viunga vya Mathare, Huruma na Eastleigh huko
Nairobi, lakini sasa anaishi maisha ya kawaida kwa kujipati riziki yeye
mwenyewe pamoja na familia yake kwa kilimo cha mjini.
Kwa hiari yake na majirani zake,
Irungu alikuwa akivunja nyumba na kuvamia na kufanya vitendo vingine vya vurugu
za uhalifu hadi Oktoba 2010. Wakati huo, polisi waliingilia kati kundi
lilipojaribu kumpiga Irungu na majambazi wengine kwa wizi wa pikipiki kutoka
mbele ya duka la bidhaa mbalimabali. Irungu alinusurika katika kundi hilo, lakini
alifungwa jela kwa mwaka mmoja.
Baada ya miezi kadhaa, wakati wa
kukutana kwa majambazi katika eneo la ujenzi, jambazi mmojawapo alipendekeza
kwamba badala ya uhalifu, wanaweza kulima ardhi ya serikali isiyolimwa katika
viunga vyao. "Tulichangishana fedha sisi
wenyewe na baadhi ya majirani walikuja na msaada wa vifaa na fedha,"
Irungu aliiambia Sabahi.
Kutoka
katika uhalifu hadi kuzalisha mbogamboga
Mwaka jana, Irungu na majambazi
wenzie wa zamani walianzisha Kikundi cha Vijana Wakulima wa Mathare, kikundi
kimojawapo kati ya vikundi kadhaa visivyokuwa rasmi ambacho kinazalisha matunda
na mbogamboga katika makazi duni. "Kwa mwezi, shamba linaweza
kunipatia zaidi ya shilingi 50,000 (Dola 590) baada ya kutoa gharama za
uzalishaji," alisema Irungu.
Muiruri Wangethi, mwenye umri wa
miaka 20, jambazi mwingine wa zamani aliyebadilika na kuwa mkulima, pia
alihukumiwa mwaka mmoja jela kwa kuiba pikipiki mwaka 2011, lakini kupitia
mpango wa serikali wa kupunguza msongamano katika magereza, aliwekwa katika
uangalizi baada ya kukaa jela miezi miwili. "Sasa tuna uwezo wa kuzihudumia
familia zetu kwa njia halali," aliiambia Sabahi. "Tunajutia sana muda
wetu tulioutumia kwa shughuli za uhalifu na tutaendelea kujaribu kwa uwezo wetu
kufidia muda tulioupoteza."
Wahalifu waliobadilishwa kutoka
katika ujambazi wamefuata njia ileile kwa kuunda umoja wa kilimo pembezoni mito
na vijito katika mji mkuu wa Kenya, alisema. Vikundi vya ushirika vinalima
matunda ya mapesheni, pilipili, miwa, vitunguu, nyanya, mahindi, maharage,
magimbi, viazi vitamu na mviringo, mihogo, koliflawa na mboga za majani ambavyo
wanaviuza katika masoko yalioko Nairobi.
Antony Macharia, mwenye umri wa
miaka 33, mhalifu aliyejirekebisha aliyejiunga katika kilimo cha ushirika
kupitia uanachama wa Kikundi cha Wakulima wa Mathare Ghetto, alisema vijana
waliojirekebisha pia wanasaidia polisi jamii."Taarifa zetu za nyuma
zisizofutika zinatufanya washukiwa wa kwanza kila uhalifu unapofanywa katika
maeneo ya jirani," aliiambia Sabahi. "Tumeamua sisi wenyewe kuhakikisha
uhalifu unapungua."
Kikundi chake chenye watu nane mara
kwa mara hufanya mikutano katika ukumbi wa mji kuwatahadharisha vijana dhidi ya
kufuata nyayo zao za uhalifu. Pia wanafanya kazi na jamii na kuwahamasisha wale
wanaojihusisha na uhalifu kuachana na mtindo huo haramu wa maisha, alisema.
Kuiweka
ardhi katika matumizi mazuri
Mkuu wa Wilaya ya Mathare Gerald
Omoke amekadiria kwamba waliokuwa wahalifu 200 sasa wamekuwa wakulima kando ya
mto badala ya kujihusisha katika uhalifu.
Ardhi ambayo vijana wanalima ilikuwa
imetengwa kwa matumizi mengine, lakini serikali inaruhusu kwa muda matumizi
hayo ya kilimo ili kuwasaidia waliokuwa wafungwa kuishi maisha ya uzalishaji na
ya uhakika, alisema."Ili kukomesha uhalifu na
shughuli za uhalifu, tunawahamasisha watu kujihusisha katika miradi yoyote
[halali] inayozalisha kipato, na kilimo ni kimoja wapo," aliiambia Sabahi.Mtindo huo unasambaa maeneo ya
jirani ya Kayole, Njiru, Ruai, Mihang'o, Dandora na Korogocho,
alisema. Baada ya maombi ya vyama vya
ushirika mbalimbali, mara kwa mara maofisa kilimo wa serikali hutembelea
mashamba kuwafundisha wakulima vijana stadi na mbinu za kuongeza mavuno ya
mazao, Omoke alisema.
Jecinta Awino, mwenye umri wa miaka
42 na muuza duka la vyakula na bidhaa huko Mathare, alisema inachukua muda
mrefu, lakini sasa wakaazi wenyeji wanatambua kwamba waliokuwa wanachama wa
kundi wamejirekebisha wenyewe. "Kuna mahitaji ya chakula na
kama mtu akipata mazao freshi moja kwa moja kutoka jirani bei inakuwa rahisi
kwa sababu hakuna gharama za usafiri zinazohusishwa," alisema. Peter Ongori, mwenye umri wa miaka
35, mkazi wa mtaa wa Kayole, alisema huduma zaozinathibitisha kufaa sana.
"Bado wanahitajika sana, sio kwa uhalifu wao wa siku za nyuma, bali kwa
mazao yao freshi," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment