Friday, February 15, 2013

On 10:26 PM by Shambani Solutions   No comments
UMOJA wa Vyama vya Wakulima wa Miwa Tanzania (TASGA) umeiomba Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuwasaidia kupata taasisi ambayo itashughulikia na kusimamia mizani ya upimaji miwa badala ya kutegemea viwanda vya kuzalisha sukari kwani walisema hawana imani na mizani ya viwanda hivyo.
Ombi hilo lilitolewa jana mjini hapa na Makamu mwenyekiti wa TASGA, George Mlingwa mara baada ya mkutano mkuu wa umoja huo ulliofanyika mjini hapa.
Alisema TASGA pia ina mpango wa kutafuta maabara itakayojitegemea ambayo wakulima wataitumia kupima kiwango cha sukari kwenye miwa na hivyo kupunguza udanganyifu unaofanywa kwenye viwanda vya sukari kwa lengo la kuwadhulumu wakulima.
Makamu mwenyekiti huyo alisema kuwa moja ya mikakati ya TASGA ni kuhakikisha zao la miwa linaboreshwa na kuongeza uzalishaji ambapo kwa sasa jumla ya tani 90,000 za miwa zipo tayari kwa ajili ya kuzalishwa sukari.
Aidha Mlingwa aliwataka viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa kuacha malumbano yasiyokuwa ya msingi badala yake wasimamie maslahi ya wakulima na kuhakikisha uzalishaji wa miwa unaongezeka sambamba na kuwahamasisha wanawake kulima zao la miwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa TASGA, Msabaha Nyembe alisema kuwa mikakati iliyopo sasa hivi umoja huo unajitegemea badala ya kuvitegemea viwanda na ili kufikia lengo hilo wamejipanga kuongeza mapato ya mkulima kwa kuongeza bei ya miwa.
Akielezea changamoto zinazoikabili TASGA mwenyekiti huyo alisema kuwa ni pamoja na kero ya kodi inayotozwa na TRA kwenye magari wanayotumia kubebea miwa wakati wa kupeleka kiwandani.

0 comments:

Post a Comment