Saturday, May 23, 2015

On 3:30 AM by Shambani Solutions   No comments
Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT), imewalipa zaidi ya Sh4.4 bilioni  wakulima wa pareto katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na Arusha kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi mwaka huu baada ya kununua tani 2,300 za zao hilo, imeelezwa.
Meneja wa PCT, Martin Oweka alisema hayo alipoulizwa hatua za kampuni yake kuondoa kero ya wakulima wa zao hilo waliokuwa wakilalamikia msimu uliopita kutokana na baadhi ya kampuni kuchukua mazao yao na kuingia mitini.
“PCT Iliwalipa fedha zote baada ya kupima sumu ya pareto ambayo mwaka huu imeongezeka ubora wake na kusababisha wakulima wapate fedha nyingi ikilinganishwa na msimu uliopita,” alisema Oweka.
Mkulima wa zao hilo katika Kijiji cha Igale, Mbeya Vijijini, Admina Mlonzi alisema wakulima waliochuma maua yaliyochanua na kuyakausha vizuri waliyauza kwa Sh2,400 kwa kilo moja jambo ambalo linaongeza kasi ya kuboresha uvunaji, ukaushaji na uuzaji ndani ya muda unaopangwa.
Vijiji vyenye wakulima waliopata fedha nyingi baada ya kuuza pareto bora ni pamoja na Itale, Igale, Nzoho na Isongole mkoani Mbeya, wakati upande wa Njombe ni Kitope, Mulondwe na vingine vipo mikoa ya Manyara na Iringa.
Mkulima Laurent Shila wa Kijiji cha Itale Mbeya Vijijini, alisema wakulima wa pareto waliofuata maelekezo ya wataalamu katika uchumaji wa maua, wamepata fedha nyingi na kuna uwezekano wa miaka ijayo wakulima wengi wakalipenda zao hilo.
Kiwanda cha pareto kilichopo Mufindi, kina uwezo wa kusindika tani 6,000 kwa mwaka, lakini mwaka huu kimepokea tani 2,300  zilizolimwa na wakulima 25,000 hivyo uongozi wa kiwanda hicho kudhamiria kuwahamasisha wakulima kulima zao hilo kwa kufuata kanuni bora ili wanufaike.

0 comments:

Post a Comment