Saturday, June 14, 2014

On 4:48 AM by Shambani Solutions   11 comments
Banda la kuku
Safari yangu ilianza baada ya kukutana na mhamasishaji aliyenitia chachu kwamba 10 x10 x 10 you become a millionea! Kwamba ukianza na kuku 10 kila mmoja akazaa 10 na hao watoto na mama zao wakazaa kila mmoja 10 unakuwa millionea! Wakubwa kuongea ni rahisi utekelezaji ukawa mgumu sana! Changamoto kuu aipatayo mfugaji wa kuku wa kienyeji ni kuzalisha vifaranga wengi na kuweza kuwakuza! Bila hivyo kundi haliwezi kukua na kukupa kipato cha uhakika!

Safari ya ufugaji niliianza kwa kununua mitetea 30 na jogoo watatu! Ilibidi nisubiri muda hadi kuku waanze kutaga! Muda ukafika kuku wakaanza kutaga kwa fujo sana! Nilikuwa na banda moja tu ambamo kuku wote walikuwa wakilala humo. Nilitengeneza viota vingi kwa ajili ya kuku kutagia. Asubuhi nilikuwa nawafungulia! Changamoto nilizoanza kupambana nazo kwanza kama mjuavyo kuku tofauti walikuwa wanataga kwenye kiota kimoja! Ilipofika wakati wa kuatamia ikawa kila kwenye kiota kimoja kuna kuku kadhaa wamebanana wanaatamia! Hali hii haipaswi kutokea kwani kuku mmoja anaweza kuwa amejilundikia mayai mengi ambayo hawezi kuyapajoto la kutosha na kuku mwingine anakuwa amekaa kando tu hana hata yai moja. Hii ilibadilika ikawa kero kubwa! Nilijua utotoaji unaweza kuathirika sana!

Ili utotoreshe vifaranga vingi kwa wakati mmoja badala ya kutumia incubator, tumia hao hao kuku. Wakianza kutaga kila siku okota mayai na kuyahifadhi mahali salama ili kuku wasiyatie joto! Kuku wengi wanapotaga kwa pamoja hufikia wakati mayai huishatumboni unakuta wamelala kwenye viota wakiwa wameatamia mayai yaliyopo au udongo tu! Kuku anaekuwa amefikia kuatamia utamjua kwani ukimshitua haondoki kwenye kiota. Kuku anaetaga ukimshitua hukimbia! Kwa hiyo kama nimepanga kutotolesha vifaranga 100 kwa mara moja nikishagundua kuwa kuna kuku 8 wameanza kuonesha dalili ya kuatamia hapo husubiri usiku ninawawekea mayai amabayo nilikuwa nimeyahifadhi. Ambapo mimi huwekea kila kuku mayai 15. Kwa hiyo kuku 8 hufanya jumla ya mayai 120. 

Kwa kuwa banda langu ni hilo moja tu kuku wengine wanaoendelea kutaga walikuwa wanaendelea kutagia kwenye viota ambavyo kuku wengine walikuwa wanaatamia! Hali hii ilikuwa inaleta tabu sana kwani ilikuwa si rahisi kutambua mayai mapya na yenye siku nyingi. Kuondoa shida hii nilinunua MARKER PEN (rangi yoyote) na siku ya kuwawekea mayai kuku ili waatamie niliyachora mduara kuzunguka yai ili iwe rahisi kuyatambua mayai mapya. Huo mchoro hauwatishi kuku na hakuna dosari yoyote. Kwa hiyo kila siku jioni ninapokuja kuokota mayai yaliyotagwa nilikuwa pia nakagua kila kiota cha kuku walioatamia na kuondoa mayai mapya. Kumnyenyua kuku anaeatamia na kuondoa yai haileti shida yoyote!
Kuku akifikia wakati wa kuatamia ukamnyima mayai hawa wanatabia kuendelea kung'ang'ania kuatamia, hapo ilibidi kutengeneza JELA! Watu wengine wanambinu tofauti kumwachisha kuku asiatamie! Mbinu ya kumtia kuku stress inafanya kazi nzuri sana! Jela inaweza kuwa ni Tega, au Box kubwa au chumba kidogo kilichopo. Ukimfungia kuku JELA bila maji wala chakula kwa kutwa mbili siku ukimfungulia akili yake huwa ni kutafuta chakula tu hakumbuki kurudi kwenye kiota! Njia hii ilifanikiwa sana na ilifanya kuendesha shughuri zangu bila bughudha! Kuna wakati JELA ilikuwa na kuku kibao hivyo unapaswa kutengeneza kibanda cha JELA. Hawa kuku wakitoka JELA hutaga mapema sana amabapo bila hivyo wangekuwa wanaatamia. 

Pia kuku wakishaatamia kwa muda wa siku 10 nilikuwa nayapima mayai ili kubaini kama kuna mayai yasiyoweza kuanguliwa! Ni rahisi sana kama una Tochi! Ukimulika yai Kwa kulizungushia vidole kiganjani kama ni yai zima linakuwa na giza kama ni yai bovu linapitisha mwanga kama yai lililotagwa siku hiyo! Jinsi ya kuzungushia vidole yai, tengeneza duara kwa vidole vyako na dole gumba kisha pachika yai katikati ya duara ili mwanga wa tochi upenye kwenye yai! Kwahiyo unaweka tochi inayowaka chini ya yai na hii ifanyike gizani au ndani ya chumba chenye mwaga mdogo. Kadri ya yai linavyokaribia kutotolewa ukilimulika huwa na giza zaidi! Ukimulika mayai toa mayai yasiyoweza kutotolewa maana hayo hutumia joto la Mama bure!

Bado ntaendelea kuwaletea makala hii kuhusu ufugaji kuku bado sijamaliza nimeona niwarushie hii kwanza kwa kuanzia. Mwenzenu nilikuwa nahangaika kufukia tanuru la mkaa nimekuta limefunguka! Si mnajua maisha jamani! Vijana tuamke na kujiingiza katika miradi hii soon tutaona mabadiliko

Makala hii iko JAMII FORUM SEHEMU YA UJASIRIAMALI. Anayetaka kujifunza zaidi aingie humo post ilianzishwa na jamaa kwa jina la KUBOTA, kuna michango mizuri sana ya watu mbali mbali, kuanzia na mada za tiba asilia kwa kuku, chanjo za kisasa, vyakula, nk nk.......kwa hisani ya shambani solutions Tanzania limited

11 comments:

 1. thanks kaka karibu ujoin blog yetu kwa habari zaidi......kuna sehemu ya kujiunga kushoto mwa blog hii..karibu tafadhali

  ReplyDelete
 2. Shukurani kwa aliyeandaa makala hii, Aysee nimeipenda sana, naenda kubadilika kwani ufugaji wa kuku nilikuwa nautafuta sn na ni ndoto yang ya siku nyingi

  ReplyDelete
 3. asante sana kwa elimu hiyo mwezi wa saba naianza kazi...

  ReplyDelete
 4. Kazi nzuri sana, hongera sana kwa mtoa mada. Amejitahidi sana kudadavua mambo. Ninavutika sana kufuga kuku wa kienyeji. Namiliki shamba kama eka 20 kijiji cha Kilimahewa kata ya Mkwechembe, tarafa ya Kimanzichana, wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani. Kwa kuanza nimepanda mipapai ekari moja na robo. Shamba lina michungwa ya asili ilipandwa zamani bado inatoa machungwa ya kutosha.Kwa mwenye kutaka kuungana nami kwa ushauri, ushirika nk. tafadhali tuwasiliane; nipo kwa moddyguyz@yahoo.com ama 0787519910.
  Natanguliza shukurani!!

  ReplyDelete
 5. Safi sanaa kwa elimu unayotoa..!! Ni vizuri ukatoa kile unachokijua, binafsi nimeipenda sanaa kwani nina mpango wa kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji.

  Itakuwa vizuri wakati mwingine ukatoa darasa kwa watu ambao ndo wanataka kuanza shughuli kama hiyo ili waweze kupata mwanga zaidi!!

  Ahsante sana kwa elimu.

  ReplyDelete
 6. Kazi nzuri sana, bila shaka ufugaji utakufanaya uachane na kazi ya mkaa ambayo haina tija katika mazingira yetu

  ReplyDelete
 7. Napenda saaaaana ufugaji wa kuku natamani nianze

  ReplyDelete
 8. wow, nimeipenda hii sana. Ila mimi nina swell, nine kinasababisha mayai kua Vinza?

  ReplyDelete
 9. Hongera kwako kwa elimu yako nzuri juu ya ufugaji bora wa kuku wa kienyeji, nimeipenda

  ReplyDelete