Sunday, June 22, 2014

On 6:58 AM by Shambani Solutions   3 comments


HIVI ndivyo anavyosema  mkulima wa nyanya kutoka katika kijiji cha Mangalali,  bwana Paschal Sichalwe  baada ya kuanza kubadili mbinu za kilimo za kizamani na kuanza kutumia mbinu za kisasa  alizozipata kupitia mafunzo yanayotolewa na mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI)

Mjasiriamali huyu mdogo anaelezea namna  ambavyo  mradi wa MUVI ulivyoonesha  njia ya kuelekea kwenye mafanikio kwa kutoa mafunzo ya kilimo bora, kuboresha njia za mawasiliano baina yao pia  jitihada zinazofanywa katika kuwaunganisha na  masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi

Mradi wa MUVI   kwa kushirikiana na viongozi wa shirikisho la  wakulima wa nyanya wamefanya ziara za ndani na nje ya nchi katika harakati za kutafuta masoko zaidi, katika hatua za awali uongozi huo umefika nchini Kenya, Malawi na hatimaye Zambia  hii ikiwa ni kwa upande wa masoko ya nje

Masoko ya ndani, mradi wa MUVI ambao  pia umeimarisha kitengo chake cha biashara na masoko wameangalia masoko ya ndani ya nchini  na kugundua kuwa kinachosababisha nyanya kushuka bei ni kukosekana  kwa taarifa za biashara na masoko kutoka katika ngazi zote.

Katika kutatua tatizo hilo tayari mtandao wa mawasilano  kutoka  mikoa yote Tanzania zitakuwa zikipatikana ili wazalishaji wa nyanya waweze kufahamu soko liliko.  Wakulima wanapopata taarifa za biashara na masoko inakuwa rahisi kwao kufanya maamuzi ya soko. Pia matumizi ya mbao  za matangazo kwa kushirikiana na redio country fm88.5 fm na Uplands redio 89.0 fm wajasiriamali vijijini wataweza kupata taarifa za biashara na masoko.

Aidha bwana Sichalwe ambaye ameanza kuvuna  nyanya alizopanda kitaalamu akitumia mbegu bora aina ya Eden inayozalishwa na Kampuni ya Monsanto anasema kuwa ameanza kuona  faida kwani mara ya kwanza ameweza kuchuma tenga 33 ilihali msimu mzima uliopita katika shamba hilo hilo lenye ukubwa wa  nusu ekari  kwa ujumla alivuna kiasi cha tenga 56 tu.

“Msimu uliopita nilitumia mbegu  aina ya  ONXL katika shamba la nusu ekari  michumo yote nilipata  tenga  56 tu lakini sasa mchumo mmoja nimewezakuchuma  tenga 33 na nategemea kuchuma kiasi cha tenga   26 katika mchumo  wa pili.” anasisistiza Sichalwe.

Msimu uliopita nilitumia kiasi cha shilingi 532,800 ikiwa ni gharama nzima ya uzalishaji  kwa upande wa pembejeo pamoja na nguvukazi,mapato ilikuwa 606000, msimu huu nimetumia kiasi cha shilingi 570,900 kwa ajili ya pembejeo na nguvu kazi nategemea kupata kiasi cha shilingi 1,045,000 Kwa mtizamo wa haraka haraka,  bwana Sichalwe ameanza kuona faida katika kilimo cha nyanya kufuatia mchanganuo huo alioufanya.

Sichalwe ambaye pia pamoja na zao la nyanya hujishughulisha na kilimo cha alizeti na mahindi, katika hatua nyingine amewezakuimarisha biashara ya kuuza bidhaa ndogondogo kwenye  kibanda chake ambapo pia anaamini kuwa kuna siku atakuwa mjasiriamali mkubwa.

Awali Sichalwe alikuwa akilima kwa mazoea bila kutunza kumbukumbu  kuanzia uzalishaji hadi sokoni lakini baada ya mradi wa MUVI kupisha hodi kijijini kwake na kufundishwa kilimo cha kibiashara na njia rahisi ya kuandaa mpango biashara sasa ameweza kutunza taarifa zake za kilimo tangu hatua ya mwanzo hadi mwisho, hapo ndipo anapoweza kubaini mapato na matumizi katika shughuli  nzima.

“Wajasiriamali wengi wanasahau kuweka kumbukumbu  za uzalisha katika  shuguli zao wanazofanya kila siku, mali bila daftari hupotea bila kujua,kila unachofanya inakupasa uandike, kuna wengine pia hujisahau wao wenyewe, mfano akipalilia nyanya mwenyewe au akipanda hujisahau katika kipengele cha malipo ile ni nguvu kazi inapaswa kulipwa na hili linawezekana kama utakuwa umeandika”anasema.

Katika hatua nyingine Sichalwe anaamini kuwa baada ya kupata mavuno mengi na yakutosha msimu huu anatarajia kuanza kilimo cha umwagiliaji  ambacho anaamini kuwa kitamkomboa zaidi.

Pamoja na mambo mengine Sichalwe  anampango  wa kuimarisha kilimo cha ufugaji kwani tayari amenunua mbuzi  5 mara baada ya kuuza nyanya.  Idadi hiyo anaona kuwa haitoshi hivyo  anategemea kuongeza kiasi hicho  hadi kufikia mbuzi 20.

Si hapo tu Sichalwe anaamini pia kwa kuzingatia mbinu za kisasa alizozipata kupitia mradi wa MUVI kufikia mwishoni mwa mwaka  atakuwa amenza ujenzi wa nyumba ya kisasa ya kuishi.

Katika kuhakikisha kuwa Sichalwe na wajasiriamali wengine wanaozalisha  nyanya kijijini hapo wanapata mafanikio,  mradi wa MUVI umemtuma ofisa masoko  wa mradi huo kuzungumza na  na wakulima wa nyanya  katika hali ya kuwaondoa hofu hususani kwenye kipengele cha masoko.

Akizungumza na wajasiriamali wa Mangalali hivi karibuni muda mfupi mara baada ya kuunda kamati ya biashara na masoko, Ofisa masoko wa mradi, bwana Fredy Mumbuli amesema, wakulima wanategemea zaidi soko la Kariakoo na Ilala.Wafanyabiashara hawa huwa wanakimbilia katika masoko haya kwa kukosa taarifa nzuri za masoko.

“wajasiriamali hupeleka nyanya kwa wingi katika masoko hayo kwa kukosa taarifa  sahihi za masoko hali inayoplekea kushuka kwa bei ya bidhaa husika,wakulima wote nchini wakishavuna hufikiria kuuza bidhaa zao Dar es salaam  jambo ambalo si sahihi hata kidogo.”alisema Mumbuli. na kuzidi kubainisha kwamba kuwa kuna wakati  kunakuwepo na uhitaji mkubwa wa nyanya Morogogo, Arusha au Dodoma  na hata wakati mwingine Iringa

Mkulima anayezalisha nyanya Morogoro akipata taarifa za soko zuri la nyanya  Iringa anaruhusiwa kufanya  biashara  vivyo hivyo na kwa upande wa mkulima wa Arusha, Kilimanjaro na mikoa mingine inayolima zao hilo.

Hili litawezekana mara baada ya kuimarisha njia za upashanaji habari kupitia  vyombo vya habari na mbao za matangazo ambazo tayari mradi wa MUVI umejenga katika kata  16 mkoani Iringa na Njombe.

Kitengo cha habari  na mawasiliano kitakuwa kikifanya kazi  kwa ushirikiano mzuri na kitengo cha biashara na masoko katika kuwapatia wakulima taarifa za biashara na masoko.

3 comments:

  1. Habari, niemeanza kilimo cha nyanya cha mafunzo kujua yanayojiri katika kilimo hicho. Ninatumia eneo la takriban robo heka.

    Naomba kufahamu kwa mujibu wa maelezo ya huyu ndugu hilo tenga ni sawa na ndoo ngapi za lita ishirini

    ReplyDelete
    Replies
    1. Habari ndugu naomba msaada wako wa elimu ya nyanya na matumizi ya madawa katika eneo la robo kwani na mimi nahitaji kulima eneo kama Hilo 0622023549 ni kijana nahitaji kujikomboa kiichumi.

      Delete