Monday, March 10, 2014

On 2:25 AM by Shambani Solutions   No comments


Mwaka 1972, Mwalimu Julius Nyerere akiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza Azimio la Iringa lililokuwa na kauli mbiu ya ‘Siasa ni Kilimo.’ Ilikuwa ni baada ya kufafanua falsafa ya maendeleo kwamba ili tuendelee tuna hitaji vitu vinne – watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Tafsiri ya maneno haya ni kwamba nguvu kazi na ardhi ni muhimu katika maendeleo ya kilimo nchini. Hadi sasa sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia nne, imeajiri asilimia 75 ya Watanzania, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo. Serikali katika awamu zake tatu zilizotangulia ilijitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalamu na kutumia wanasiasa katika majukwaa yao ili kuhimiza kilimo ambacho mpaka sasa hakina mafanikio ya kuridhisha.

Hivi karibuni kulikuwa na maadhimisho ya mwaka wa kilimo kwa Afrika, uliofanikishwa na Jukwaa la Kilimo (Ansaf) naTaasisi ya One ya Afrika Kusini, uliofanyika Kijiji cha Kaning’ombe wilayani Iringa, Mkoa wa Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, alikutana na kuzungumza na wakulima.

Mkulima wa mfano
Mkulima Eusebio Mbangile alipewa nafasi ya kuonyesha shamba lake kwa Dk. Ishengoma hivyo kuwa mfano wa utekelezaji wa Azimio la Siasa ni Kilimo. Baada ya kusota na kilimo kisichokuwa na tija kwa muda mrefu, Mbangile ameibukia kuwa mkulima mwenye mafanikio baada ya kufuata ushauri wa kitaalamu akiwa na shamba la ekari 46 ambalo amepanda mahindi na miche ya matunda. Mbangile anasema shamba lake ameligawa katika vitalu vitatu na kitalu cha kwanza amepanda mahindi ambayo anatazamia kupata magunia 25 kwa ekari moja.

“Eneo hili la pili lina ukubwa ekari nane ambalo analima bila kuweka mbolea ya kukuzia. Natarajia kupata gunia 15 hadi 16 kwa ekari moja.Nikiweka tofauti ya eneo la kwanza na la pili, naona hapa mazao yanapungua,” anasema Mbangile. Eneo la tatu ambalo lina ekari 3.5, mkulima huyo ametumia Sh1.7 milioni kuandaa shamba hilo.

Anasema sababu ya kuyagawa mashamba hayo ni kujiweka mbali na hasara ambayo inaweza kutokea kwenye shamba, lakini mengine yatakuwa salama. Mbali na mahindi, Mbangile pia amelima miche ya matunda kama vile maembe miti 37, machungwa miti 35, maparachichi miti 79. Mkulima huyo anasema kwa jumla ametumia Sh3.9 milioni ikiwa ni gharama za kuandaa shamba lote ikiwa ni pamoja na mbolea alizotumia ambazo ni Minjingu mazao, urea na Can na mbegu za hybrid 625 kwa kitalu cha kwanza, hybrid 614 kwa kitalu cha pili na mbegu ya asili kwa kitalu cha tatu.

Anasema amepata mafunzo ya kilimo kutoka kwa wataalamu wa kilimo wa kijiji, semina za kilimo kwa wafadhili Dai Pesa, Global Sasa kama 2000 ambao walikuwa na mtaji ulioniwezesha kupandia mazao yangu kwa mbolea za Urea, NPK kupata magunia 23 kwa ekari, ikiwa ni mara ya kwanza. “Kwa sasa tunasaidiwa na Shirika la Rural and Urban Development Initiatives (Rudi).

Mafanikio na changamoto
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Mbangile mwenye wake wawili na watoto 13 anasema amefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa na anamudu mahitaji ya familia yake. Pamoja na mafanijio hayo bado ana ndoto kubwa zaidi.

“Ninapata magunia ya mahindi 102 kwa wastani wa gunia 26 hadi 27 kwa ekari moja. Kwa mwaka huu natarajia kupata Sh12.7 milioni baada ya kuuza mazao yangu. Nikizipata nataka nifanye mipango ya kukopatrekta kwa ajili ya kupanua shughuli za kilimo,” anasema Mbangile. Anasema changamoto anazopata ni pamoja na ukosefu wa masoko, miundombinu mibovu na mitaji.

Kijiji cha hamasika
Akizungumzia mafanikio ya kilimo kijijini hapo, Mwenyekiti wa Kijiji, Paschal Mfunda anasema: “Mimi nina rekodi ya kilimo kama Mbangile. Tulianza tangu tukiwa vijana kwa kilimo cha nyanya na tulikuwa tukisafirisha kwenda Dar es Salaam. “Hadi sasa tunalima kwa mashindano. Kwa msimu mmoja tumevuna nyanya matenga 80 na kuuza. Nina hali nzuri tu.”

Naye Bwana Kilimo wa kijiji, Fati Hamad Msigwa anasema anahudumia zaidi ya wakulima 900 kijijini hapo, lakini anafarijika kuona wakulima wakubwa kama Mbangile ambao idadi yao imefika 10.

Suluhisho la wakulima Akizungumzia suluhisho kwa wakulima katika upatikanaji wa pembejeo, Ofisa Kilimo Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu anasema wamekuwa wakiwaunganisha wakulima katika vikundi ili wapate mikopo. “Tumekuwa tukiwaunganisha kwa njia ya vyama vya kuweka na kukopa (saccos) ili wapate mikopo. Wakulima wengi vijijini wana hati za kimila ambazo haziwawezeshi kupata mikopo ya benki. Tayari tuna vikundi tunavyoviwezesha kupata mikopo,” anasema Nyalu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Beatus Malema anasema Serikali imefikia hatua nzuri katika kuanzisha benki ya wakulima na bado kuna fursa za kukopa. Naye Dk. Christine Ishengoma anasisitiza muungano wa wakulima kwa lengo la kuinuka kiuchumi.

Mazao yanayolimwa ni mahindi, maharage, ufuta, karanga, mpunga, tumbaku, soya na mtama. Kati ya mazao hayo ni kiasi kidogo tu husindikwa, huku sehemu kubwa ikiuzwa yakiwa ghafi. Mkoa wa Iringa una wilaya za Mufindi, Iringa na Kilolou na kaya zipatazo 158,713.

0 comments:

Post a Comment