Monday, March 10, 2014

On 2:43 AM by Shambani Solutions   No comments
Kilimo cha korosho nchini kinatarajiwa kuchukua sura mpya baada ya kutokana na kuwepo kwa mpango wa kujengwa kwa viwanda vitatu vya kubangua korosho vitakavyoongeza thamani ya zao hilo. Lakini si hayo tu bali pia wakulima watanufaika zaidi kwa kuwa korosho zitakuwa zikibanguliwa hapa nyumbani badala ya kusafirishwa nje ya nchi zikiwa ghafi.

Akizungumza na gazeti la The Citizen, wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma alisema viwanda hivyo vitajengwa katika Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Mkuranga na Tunduru na vitaanza kazi mapema mwaka huu. Juma alisema fedha za ujenzi wa viwanda hivyo zitatolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Korosho Tanzania, lakini hakufafanua gharama za ujenzi. Mbali na hayo Juma anawataka wakulima kuandaa vizuri kurosho ili wapate bei nzuri sokoni. “Kwa bahati mbaya, baadhi ya wakulima ambao si waaminifu wamekuwa wakichanganya korosho na maji kwa ajili ya kuongeza uzito. Tabia hii haikubaliki kabisa kwani inawakatisha tamaa wanunuzi na kushusha thamani ya korosho yetu,” anasema mkurugenzi huyo.

Hivi sasa Tanzania inakadiriwa kubangua asilimia mbili tu ya korosho yote nchini na kiasi kinachobaki kinauzwa nje kama mali ghafi pamoja na kuwepo kwa mipango hiyo. Pamoja na kuwapo kwa mipango hiyo Tanzania inatajwa katika Bara la Afrika kuwa katika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa zao hilo, ikifuatiwa na Nigeria. Lakini kilimo cha korosho kimekuwa kikikabiliwa na matatizo mengi ambayo mpaka sasa hayajatatuliwa. Moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa viwanda vya kubangulia korosho na kusababisha wakulima kuuza korosho ambazo hazijabaguliwa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na the Agricultural Non State Actors Forum (ANSAF) mwaka 2008, kuuza korosho nje ya nchi bila kubanguliwa kuna hasara zake kwani wakulima wamekuwa wakipata kipato kidogo huku serikali ikikadiriwa kupoteza dola 110 milioni, kila mwaka. Utafiti huo ulipewa kichwa cha habari. “Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara ya Korosho Tanzania”. “Vikwazo vya kujenga viwanda vya kubangua korosho nchini, vimesababishwa na udhaifu wa sera, ukosefu wa fedha na kutokuwapo kwa uzoefu katika soko la kimataifa,” sehemu ya utafiti, inaeleza.

Katika kipindi cha mwaka 2007 na 2012, zaidi ya tani 461,000 za korosho ghafi ziliuzwa nje ya nchi kwa gharama ya dola ya Sh85 milioni sawa na Sh136 bilioni. Mtaalamu Mshauri wa kimataifa, Jim Fitzpatrick na mwenye uzoefu wa miaka 30 katika zao hilo, anabainisha kuwa kutokuwapo kwa mazingira mazuri ya soko ni moja ya matatizo yanayowaathiri wakulima wa Tanzania. Fitzpatrick anaeleza kuwa wakulima wanaofanikiwa kubangua korosho nchini, wamekuwa wakinufaika zaidi kuliko ambao wanauza korosho ghafi nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya ANSAF, kama korosho ghafi zilizouzwa nje nchi, zingeliuzwa zikiwa zimebanguliwa, wakulima wa korosho wangepata dola 750 za Marekani sawa na Sh1.2 trilioni. Fitzpatrick anasema fedha ambazo wakulima wanapokea ni kati ya asilimia 57 na 65 ya mauzo ikiwa ni bei halisi ya kuuzia korosho huku wakipunjwa karibu asilimia 15 kutoka katika bei elekezi ya Bodi ya Korosho.

“Gharama ya thamani ya korosho nchini haiendani kabisa ukilinganisha na za nchi nyingine. “Kwa korosho inayouzwa India, mkulima anapata kiasi kidogo, ukilinganisha na soko la kimataifa kutokana na kuwapo kwa gharama kubwa za kodi, usafirishaji na gharama za wanunuzi wanaounua kwa mnada. Kutokana na hali hiyo mkulima wa Tanzania hapati bei inayofanana na korosho anayozalisha, ukilinganisha na wakulima wa Afrika Magharibi ambao soko lao liko wazi,” anasema Fitzpatrick.

Kwa upande wake, Juma anasema malalamiko sugu ambayo yalikuwa yakitolewa mara kwa mara, sasa yamepungua kutokana na usimamizi mzuri wa zao hilo na kutoa elimu kwa wakulima. Kwa muda wa miaka minne sasa kumekuwapo kwa malalamiko sugu kutoka kwa wakulima, kutokana na kutokuwapo kwa taarifa sahihi za maendeleo ya zao hilo. “Kutokana na kanuni za mwaka 2009, mkakati wa kutatua matatizo ya wakulima yako katika hatua ya utekelezaji. Licha kuwa na wataalam wachache, kutokana na msaada wa bodi ya korosho, mambo yanakwenda vizuri,” anasema Juma. Anasema hivi sasa kuna wilaya 42 zinazolima korosho wakati nchi nzima ina wataalam 70. “Unategemea wataalamu wachache hivyo kukagua wilaya zote 42? Wanaweza kufanya hivyo kama watapata msaada kutoka kwa wadau wengine,” anasema.

Takwimu zinaeleza kuwa mahitaji ya korosho duniani yanakuwa kwa asilimia 8 kila mwaka, ikiwa ni ishara kwamba Tanzania inapaswa kuimarisha uwekezaji wa zao hilo.

0 comments:

Post a Comment