Saturday, January 4, 2014

On 12:54 AM by Shambani Solutions   No comments
Serikali imetakiwa kuwekeza zaidi  katika kilimo na kuandaa mipango na sera zitakazowanufaisha wakulima wa ngazi ya chini.
Rai hiyo ilitolewa juzi na baadhi ya wataalamu walipokuwa wakizungumza katika warsha ya  kujadili ripoti ya maendeleo ya watu  katika mwaka 2013.
Ripoti hiyo kuhusu uchumi, imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP). Baadhi ya wataalamu hao wa uchumi walisema ingawa taifa limefanikiwa kugundua  gesi na mafuta lakini ukuaji wa uchumi katika mwaka 2014, kwa kiasi kikubwa utategemea kilimo.
Walisema sekta hiyo ndiyo inayotegemewa na Watanzania wengi na kwa hiyo lazima ipewe kipaumbele. Mtaalam wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humprey Moshi, alisema ili sekta hiyo iwe na matokeo makubwa, lazima kuwe na mkakati wa kuwekeza.
Alisema uwekezaji huo unapaswa kwenda sambamba na mipango ya kuwasaidia wakulima wa ngazi ya  chini ili waweze kunufaika na kilimo. “Kinachotakiwa kutiliwa mkazo mwaka huu ni kuwekeza zaidi kwenye kilimo na  kutengeneza mipango na sera zitakazosaidia kundi la wakulima wa kawaida ambao ndiyo wengi kuliko wakulima wakubwa,”alisema Profesa Moshi.
Alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuweka mkazo katika kilimo cha umwagiliaji ili kuepusha nchi katika hatari ya kukumbwa na njaa kali. “Bado wakulima wanategemea mvua ambazo  zisiponyesha,  kuna hatari ya kuingia kwenye njaa, nimepita maeneo mengi na kuona yakiwa makavu kabisa watu hawajalima”alisema .

0 comments:

Post a Comment