Sunday, December 15, 2013

On 1:15 PM by Shambani Solutions   No comments
Mawakala wanaonunua pareto kwa niaba ya Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) mkoani Mbeya, wameagizwa kufanya kazi yao bila kukopa wakulima ili kuepusha kero.
Meneja Mkuu wa PCT, Martin Oweka alitoa agizo hilo jana kwa simu kwamba, kampuni itahakikisha wakulima wa pareto hawakopwi wala kupunjwa kwenye mizani.
Oweka alisema kampuni yake inazo fedha za kutosha na kamwe haitakubali wakulima walalamike kuhusu kukosa fedha za pareto na kwamba, wanachotakiwa ni kuboresha kilimo ili waweze kupata fedha nyingi.
Nawasihi wachume maua yaliyochanua, wayakaushe vizuri na ndani ya siku 10 wayauze ili yawe na ubora na kuwapatia fedha za ziada’’, alisema.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini Ipyana Seme alidai wakulima wa zao hilo Kata za Ilembo na Iyunga Mapinduzi walilalamika kukopwa pareto yao.Seme alisema madiwani wa kata hizo wanayo orodha ndefu ya wakulima wanaolalamika.
Hata hivyo diwani wa Kata ya Ilembo Patrick Mwasenga na wa IyungaMapinduzi, Babeli Yilimo walikanusha taarifa hizo wakisema hawajapokea malalamiko hayo.
Meneja wa PCT, alisisitiza kwa njia ya simu akisema kuwakopa wakulima ni dhambi na kwamba kampuni yake haitakubali tukio kama hilo likitokea. Aliwataka mawakala wanaonunua pareto kwenye vijiji kuzingatia utaratibu wa kampuni ikiwa ni pamoja na kuwapatia risiti wakulima wanaouza pareto ili waweze kupata malipo ya pili kwa uhakika.

0 comments:

Post a Comment