Monday, October 14, 2013

On 6:53 AM by Shambani Solutions   No comments


Mvomero. Wakulima wanaokadiriwa kufikia 500 wanaolima katika Bonde la Mgongola lililopo wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wamefunga barabara ya Turiani –Morogoro katika eneo la Mkindo kuanzia majira ya saa 11 alfajiri wakishinikiza kuonana na Mkuu wa Mkoa huo Joel Bendera ili afike kuwatatulia mgogoro wa muda mrefu baina yao na wafugaji.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero Anthony Mtaka,akiongoza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo,walifika katika eneo hilo kwa nia ya kuzungumza na wakulima hao waliokuwa na hasira, ambao hata hivyo walimkataa wakitaka kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ili awatatulie mgogoro huo.
Wakulima hao walifunga barabara hiyo na kurusha ovyo mawe na fimbo hali iliyowafanya polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi baridi hewani ili kuwatuliza wananchi hao bila mafanikio.

Kitendo hicho cha kurusha mawe kilisababisha kuvunjika vioo kwa gari la Mkurugenzi wa halamashauri wa wilaya ya Mvomero na mkuu huyo wa wilaya, ambapo askari wa jeshi la Polisi Pc Nelson alijeruhiwa sehemu ya mdomoni na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwaajili ya matibabu.

Kufuatia vurugu hizo, Mkuu wa wilaya ya Mvomero Anthony Mtaka aalikemea tukio hilo la wananchi kufunga barabara inayotumiwa na wasafiri mbalimbali wakiwemo watu ambao wanashiriki shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, wagonjwa na watu wengine, na kwamba kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa vikali na kila raia mpenda amani na utulivu.

Mkuu huyo wa wilaya alieleza pia kukerwa na kitendo cha wananchi hao kurusha ovyo mawe na kumjeruhi askari na hata kuvunja vioo vya magari ya viongozi, waliokwenda eneo hilo kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinakuwepo, ikiwemo amani kwa kundi hilo la wakulima.

Hadi waandishi wa habari wanaondoka eneo la tukio polisi waliondoka ili kujipanga upya kwenda kufungua barabara hiyo na kudhibiti vurugu za wakulima hao.
Vurugu za wakulima na wafugaji katika maeneo mbalinbali ya mkoa wa Morogoro hususani wilaya za Mvomero na Kilosa, yamekuwa ni wimbo wa muda mrefu unaohitaji jitihada za pamoja za wadau katika kuhakikisha yanamalizwa kutokana na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

0 comments:

Post a Comment