Friday, October 18, 2013

On 1:07 PM by Shambani Solutions   No comments
 Nachingwea. Wakulima 26 wa kata za Nambambo na Nachingwea, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi wamefungua kesi ya madai wakitaka Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nambambo kuwalipa Sh22.9 milioni zilizosalia kutokana na malipo ya mauzo ya zao la korosho za msimu uliopita ambapo walilipwa pungufu ya bei dira waliyokubaliana.

Katibu wa kamati inayofuatilia madai hayo, Ahmadi Majali alisema wakulima hao wamefungua mashtaka hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea wakitaka chama hicho kiwalipe kiasi hicho cha fedha zilizosalia kutokana na malipo ya korosho zenye uzito wa kilo 163,947 zenye thamani ya Sh77.2milioni walizokiuzia chama hicho msimu uliopita.
Majali alisema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya juhudi za kutaka suala hilo kumalizwa nje ya mahakama kushindikana, huku kukiwa hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuwa zitalipwa wakati msimu mpya wa mauzo ya zao hilo ukitarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alibainisha kuwa chama hicho kimekiuka makubaliano ambayo yapo kwenye stakabadhi za mauzo ambazo zinaonyesha wangelipwa kiasi chote cha Sh1200 kwa kilo na kuwa uamuzi wa kukishtaki chama hicho unatokana na kuwa ndicho walichokiuzia korosho zao na si Chama Kikuu cha Ilulu.
Mwenyekiti wa chama hicho cha ushirika cha msingi cha Nambambo, Sadiki Kachambila alikiri chama chake kufikishwa mahakamani wiki ijayo na kudai kuwa wao walikuwa ni mawakala na wa mazao kwa wakulima na kuwa wanaostahili kufikishwa mahakamani ni chama kikuu cha Ilulu.

0 comments:

Post a Comment