Wednesday, October 9, 2013

On 12:22 PM by Shambani Solutions   No comments
Idara ya Kilimo Mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Chuo cha  Kilimo Uyole mkoani Mbeya, imeanza kutekeleza  agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuutaka mkoa huo utenge maeneo kwa ajili ya  kilimo cha mbogamboga na matunda ili kuinua pato la wananchi na mkoa kwa jumla.
Ofisa wa kilimo wa mkoa huo, Enock Nyasebwa, alisema utekelezaji huo unahusisha kuanza kutafuta maeneo maalumu ya skimu za bustani kwa ajili ya kilimo hicho.Alisema mkakati mwingine ni kuwaunganisha  wakulima  katika chama kimoja cha  ushirika,  kufanya tathimini ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda  na kuwapo kwa soko la uhakika.
Nyasebwa alisema mikakati  mingine ni kuhakikisha kuwa mkoa unajenga maghala  na  vifaa maalumu vya kuhifadhia mbogamboga, ili zisiharibike  wakati zinasubiri soko.Alisema ili kufikia malengo hayo, idara yake itaanza kutoa elimu kwa wakulima, kujiunga katika vikundi ili kufikia malengo ya Serikali.
Akitoa maoni yake, mkulima wa mbogamboga  katika Kata ya Ilolo, jijini Mbeya,  Athamas Joram, alipongeza jitihada za Serikali katika kuwakwamua wakulima na kwamba mikakati  hiyo ilenge kuwafikia wakulima wote ili waweze kunufaika.

0 comments:

Post a Comment