Thursday, September 19, 2013

On 1:52 PM by Shambani Solutions   No comments
Kwa miaka mingi sekta ya kilimo nchini imekuwa ikitajwa kuwa ‘uti wa mgongo’ wa uchumi wa taifa, lakini imebainika baadhi ya sera za kilimo zinapunguza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo. Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ushirikano na Taasisi ya Utafiti wa mambo ya Uchumi na Kijamii (ESRF), imebainisha kuwa mfumo wa malipo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya biashara unapaswa kupitiwa upya kwa kuwa unawanufaisha wafanyabiashara pekee. Ripoti inayoainisha ufanisi wa chakula na sera za kilimo Tanzania kuanzia mwaka  2005 hadi 2011 inabainisha kwamba serikali inajipanga kuupitia upya mfumo wa stakabaadhi ghalani ili uwanufaishe wakulima.

Wakulima korosho wanapunjwa
Mkurugenzi Sera na Mipango Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Nkuvililwa Simkanga anasema kwamba wafanyabiashara wa korosho wamekuwa wakipanga bei na kuwaumiza wakulima wa zao hilo.Simkanga anasema kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo wakulima wamekuwa wakishindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
Ripoti hiyo itatumika kuongeza uwezo wa wizara kuchambua sera za kilimo zilizopo ili kuandaa sera nzuri zitakazo mnufaisha mkulima. “Wakati tunaanzisha sera fulani kunakuwa na changamoto zinazojitokeza, hivyo kama wizara tuko tayari kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mfumo w stakabathi ghalani kwa wakulima wetu wa korosho ambao wanaonekana kunufaika kidogo,” anaelezea Simkanga.
Mkurugenzi Mkuu wa ESRF, Dk Bohela Lunogelo anasema ripoti hiyo ililenga kubaini namna sera za kilimo na chakula zinavyotekelezwa, jinsi zinavyoweza kuwa kikwazo au kuleta manufaa kwenye sekta hiyo. Lunogela anasema ingawa mfumo wa stakabadhi wa mazao ghalani umesaidia wakulima wa mpunga na mahindi kuuza mazao yao kwa bei ya juu, mfumo huo una udhaifu katika zao la korosho. “Wakulima wa mpunga wananufaika na mfumo huu, lakini wakulima wa korosho bado wanaumia kwasababu  wanunuzi ni wachache, hivyo wanajipangia bei pasipo kuwa na ushindani wa kutosha, mwisho wa siku mkulima ndiye anayeumia,”anasema Lunogelo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia anasema kwamba kodi ya kusafirisha mazao nje ya nchi (Export levy) imeanzishwa ili kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kubangua korosho.

Ghasia aliwaambia wadau wa kilimo kuwa kodi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwahamasisha wafanyabishara kusafirisha korosho ambazo tayari zimebanguliwa ili kuziongezea thamani na kuuzwa kwa bei ya juu. “Tukiwa na viwanda vya kubangulia hapa nyumbani, ajira kwa vijana wetu itaongezeka, lakini katika kodi hiyo tulizingatia thamani ya korosho zilizobanguliwa hivyo tulianzisha ili kuwabana wanaosafirisha korosho ambazo hazijabanguliwa,”anaeleza Ghasia.
Ghasia anaeleza kwamba wadau wengi wamekuwa wakizungumzia kodi zinazotozwa na halmashauri na kusahau kuangalia kodi zinazotozwa na vyama vya ushirika ambavyo havitoi msaada mkubwa kwa wananchi.“Kodi za halmashauri zina kwenda kwenye huduma za shule, afya na sehemu nyigine za kijamii ambazo humgusa mkulima moja kwa moja, tofauti na kodi zinazotozwa na vyama vya ushirika. Kama tunataka kumpunguzia kodi mkulima, tuziangalie kodi zote ili tuone tunamsaidiaje mkulima,”anafafanua Ghasia.
Mwanzoni mwa mwaka huu, wakulima wa korosho mkoani Mtwara walilalamikia mfumo wa stakabadhi ghalani kwamba wafanyabishara walikuwa wakinunua korosho chini ya bei iliyopangwa na serikali kwa kisingizio walipata hasara msimu wa mauzo uliopita.
Ripoti hiyo imekwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa wakulima wa pamba wanatozwa kodi wastani wa asilimia 30 na kuwapunguzia uwezo wao wa kuwekeza katika zao hilo.“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapaswa kupunguza mzigo wa kodi kwa wakulima wa pamba kama njia ya kuwavutia wakulima wengi zaidi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kodi
Kuhusu kodi inayotozwa kwa waingizaji wa sukari nchini, ripoti imeonyesha wateja wa bidhaa hiyo wanalipa bei kubwa zaidi ikilinganishwa na bei za kimataifa.Imeelezwa kwamba wakulima wa sukari hawanufaiki na vizuizi vya sukari vilivyowekwa mipakani na kwamba kinachoonekana ni kuwatenga na mabadiliko ya sera za biashara ambayo yangeweza kuwainua kimaendeleo.
Serikali imetakiwa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya sukari, ili kuruhusu na kuziwezesha kampuni kuwalipa wakulima wa sukari bei wanayostahili kulipwa. Ripoti hiyo imeeleza pia uzalishaji wa sukari nchini ulikuwa kwa asilimia 17 kutoka tani 2.3 milioni mwaka 2005 hadi tani 2.7milioni mwaka 2010. Jumla ya tani 377,313 za sukari ambazo ni sawa na asilimia 23, zilitimika viwandani mwaka 2009/2010, huku asilimia 77 iliyobaki ikitumika kwa matumizi ya kawaida. Pia, ripoti hiyo imebainisha kwamba hatua ya serikali kuzuia usafirishaji wa mahindi kwenda nje ya nchi ili kupunguza bei na kulinda zao hilo, mpango huo haujafanikiwa kama ilivyotegemewa awali. “Zuio la kuuza mahindi nje halikusaidia kukuza soko la ndani kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo yalikuwa na mahindi mengi huku sehemu nyingine zikiwa na uhaba wa zao hilo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

0 comments:

Post a Comment