Tuesday, August 6, 2013

On 5:23 AM by Shambani Solutions   No comments

Bill Clinton akiwa na Rais Kikwete katika kukagua miradi inayosimamiwa na taasisi

Dar es Salaam. Taasisi ya Clinton Foundation imetiliana saini mkataba wa makubaliano ya kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kuwajengea uwezo wakulima wadogo na kuzalisha mbegu bora nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Sophia Kaduma alisema kuwa uwekaji saini huo ulifanyika katika viwanja vya Ikulu, Agosti 3 mwaka huu, mbele ya Rais Jakaya Kikwete na mwanzilishi wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais mstaafu wa Marekani Bill Clintoni.

“Makubaliano yaliyosainiwa ni muhimu sana kwa sekta ya kilimo nchini, kwani yatachangia katika utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuendeleza Tasnia ya Mbegu na kuongeza upatikanaji wake,kama mojawapo ya pembejeo muhimu kwa kufikia angalau tani 60,000 kutoka tani 30,000 wakati mahitaji ni tani 120,000,” alisema.


Alifafanua kuwa taasisi hiyo ya Clinton imeazimia kusaidia wakulima wadogo kuzalisha kwa tija ili kupata chakula cha kutosha, pia kusaidia kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani kama vile maua na mbogamboga na kuendeleza teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji


Kaduma alisema kuwa kwa kuanzia, taasisi hiyo itahusika katika uzalishaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (Asa), hatua ambayo itawezesha kupunguza tatizo la upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima tofauti na ilivyo sasa ambapo hutegemea zinazoagizwa nje ya nchi.


“Itaanzia katika shamba la mbegu la Wakala wa Mbengu za kilimo lililopo Dabaga wilayani Kilolo-Iringa, ambalo lina ujazo wa tani 1,000 ambazo ni hekta 960, awali ilikuwa inazalisha mbegu hizo kwa hekta 150, pia wakulima jirani na eneo hilo watapata fursa ya kujifunza mambo mengi,” alisema.


Alisisitiza wizara yake inaamini kwamba hatua hiyo ambayo inatarajiwa kuanza wiki tatu zijaz, itabadilisha mwelekeo wa wakulima wengi ambao wamekuwa na tabia ya kutumia mbegu ambazo ni sehemu ya mazao yao waliyovuna ambazo hazina ubora, hivyo wanapopanda wengi huvuna chini ya kiwango.

0 comments:

Post a Comment