Wednesday, February 13, 2013

On 4:08 AM by Shambani Solutions   2 comments
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh Abdallah Kigoda

HAKUNA mpango wa kukifufua Kiwanda cha Zana za Kilimo Mbeya (ZZK) kilichogeuzwa kuwa cha kutengenezea bia za Serengeti.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, alitoa jibu hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ileje, Aliko Kiboma (CCM), aliyetaka kujua kama serikali ina mpango wa kufufua kiwanda hicho cha zana za kilimo.

Alisema, kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa njia ya ufilisi mwaka 2002 kutokana na mtaji mdogo uliokuwa umewekezwa, utendaji usioridhisha wa kiwanda na deni la Benki ya NBC.

“Kampuni ya CMG Investment inayomiliki kiwanda hicho, ilifanya tathmini kwa lengo la kukifufua ili kuendelea na uzalishaji wa zana za kilimo, lakini ilibaini faida isingepatikana kama angeendelea na uzalishaji wa zana za kilimo”.

Alisema, faida isingepatikana kutokana na changamoto zilizokuwapo awali ikiwamo ya teknolojia kupitwa na wakati, ukosefu wa malighafi ya chuma, gharama za usafirishaji wa malighafi kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ushindani wa kibiashara hasa baada ya zana nyingi za kilimo kuanza kuingizwa kutoka nje ya nchi na kwa bei nafuu.

“Baada ya kufanya tathmini hiyo, mwekezaji aliomba kibali cha kubadilisha biashara na sasa anatarajia kuanza uzalishaji wa bia aina ya Serengeti.

“Aidha, mwekezaji aliona kuanza kuzalisha bia ataweza kutoa ajira nyingi kwa wakazi wa Mbeya na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la serikali kupitia kodi atakazolipa.”

Akijibu swali la nyongeza, lililotaka kiwanda hicho kifufuliwe baada ya chuma kupatikana Liganga, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Abdallah Kigoda alisema pamoja na chuma hicho kupatikana bado uchimbaji wake haujaanza.

2 comments:

  1. Hehee, kwamba wanasubiria chuma kianze kuchimbwa ndo waanze mipango ya kujenga kiwanda. Sijui nani alituroga hakyanani.

    ReplyDelete
    Replies
    1. cha kujiuliza zaidi hapa kwa huyu aliyepewa hiko kiwanda hakujua hiyo changamoto ya chuma? kama aliona hawezi si angeacha wengine wawekeze....ni usanii tu wa wawekezaji wetu wakishirikiana na baadhi wa wajanja serikali napata mashaka sana juu ya KILIMO KWANZA

      Delete