Tuesday, February 26, 2013

On 1:00 PM by Shambani Solutions   No comments


Vijana wa JKT wakiwajibika kibaha
ZAIDI ya hekta 500 za ardhi zilizogeuka kuwa shamba pori kwa kipindi kirefu Kibaha Pwani, zimefufuliwa na vijana wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 832 .

Kufufuliwa kwa hayo mashamba hilo kumeelezwa kuwa kutarahisisha upatikanaji wa chakula kwa askari waishio katika kambi hiyo pamoja na wale watakaokuwa wanapita kwa ajili ya kupata mafunzo ya kijeshi.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni kwenye mahafali ya wahitimu wa mafunzo ya awali ya jeshi hilo yaliyopewa jina la Operation Sensa 2012-2013 yaliyofanyika kwenye viwanja vya mabatini Kibaha wakati wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi.

Walisema kutokana na mafunzo waliyoyapata kwa kipindi cha miezi sita wakiwa kambini hapo pamoja na mambo mengine,wameweza kupata uelewa wa namna ya kuendesha kilimo cha kisasa,ujasiriamali,uzalendo pamoja na upendo na ushirikiano katika kufanya kazi.
Aidha walisema kuwa mafunzo waliyoyapata yatakuwa kichocheo kikubwa kwao mahali popote watakakokwenda na kuahidi kuwa watakuwa tayari kuitumikia nchi yao na kuhakikisha kudumisha amani iliyopo.

Kwa upande wake, Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Brigedia Jenerali Mwanamakala Kilo ambaye ni Mkurugenzi kutoka Suma Jkt,aliwataka vijana hao kutojihusisha na tamaduni za kigeni ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwaharibu vijana wengi kitabia na badala yake wajijengee staha katika uvaaji wa mavazi na vitendo vinavyokubalika na jamii.

Alisema kuwa hivi sasa vijana wengi wamejiingiza kwenye tamaduni za kigeni kwa kufanya vitendo visivyokubalika na jamii ya Mtanzania na kwamba hali hiyo ni lazima ipigwe vita kwa nguvu katika maeneo yote.

“Utamaduni wa kigeni ambao hauleti sura nzuri ni sawa na bidhaa bandia isiyokubalika hapa nchini,nawaomba huko muendako ili muendelee kuwa vijana wanaokubalika ni vema mkajiepusha na kujiingiza katika kundi hilo”Alisema

Kambi ya Ruvu JKT ni miongoni mwa kambi za jeshi kongwe ambazo zinazalisha vijana wengi kwa kuwapa mafunzo ya kijeshi na kwamba katika mahafali hayo vijana wapatao 989 kati yao wavulana 754 na wasichana 240 wakiwa na viwango vya elimu mbalimbali walihitimu.

0 comments:

Post a Comment