Saturday, April 27, 2013
On 6:14 AM by Shambani Solutions No comments
Ugonjwa hatari unaoshambulia mahindi na kusababisha saratani kwa binadamu
umeingia nchini na wakulima sasa wametahadharishwa kutokula mahindi hayo wala
unga ambao haujakobolewa.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huo huota 'fungus' ambao ina sumu
inayoitwa 'Aflatoxin' ambayo inaweza kusababisha madhara kwa wanyama na
binadamu hususan ugonjwa wa saratani. Mbali na kutikisa mikoa kadhaa na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima,
ugonjwa huo ambao umeanzia nchini Kenya unaendelea kusambaa kwa kasi na sasa
umeingia pia nchini Uganda.
Awali ugonjwa huo uliripotiwa kuzikumba wilaya za Babati mkoani Manyara na
Meatu mkoani Shinyanga tu, lakini sasa umesambaa hadi katika mikoa jirani
ikiwamo Kilimanjaro
.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama jana alilithibitishia gazeti hili
kuwa mkoa wake umekumbwa na ugonjwa huo na tayari umesambaa katika wilaya tatu;
Moshi Vijijini, Siha na Hai. "Ni kweli baadhi ya wilaya zimekumbwa na
ugonjwa huo, bahati mbaya sana hauna tiba na unasambaa kwa kasi... Wataalamu
wanaendelea kuwaelimisha wakulima kutambua dalili zake," alisema Gama.
Gama alisema endapo mkulima atabaini shamba lake kushambuliwa na ugonjwa huo
katika hatua za awali, anachotakiwa kufanya ni kung'oa mimea yote ya mahindi na
kuichoma moto.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga alisema takriban hekari 14
zimeshambuliwa na ugonjwa huo katika shamba la Watawa wa Kanisa Katoliki
Mailisita na shamba la mkulima wa Lambo. Alisema tayari wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Selian
(SARI) ya Jijini Arusha wamefika wilayani humo na kutoa tahadhari kwa wakulima
juu ya athari za ugonjwa huo. Mfanyabiashara mashuhuri wa mjini Moshi, John
Bennett anayemiliki mgahawa wa Golden Shower aliitaka Serikali kutoa elimu kwa
wananchi na wafanyabiashara na kuchukua tahadhari.
"Utajuaje unga wa dona haukutokana na hayo mahindi au pumba ya chakula
cha mifugo hayakutokana na hayo? Hili jambo ni zito sana si la kufanyia utani
hata kidogo"alisema Bennett.
Mkulima wa Kijiji cha Kikavu Chini wilayani Hai, Justine Mvungi alisema
wataalamu kutoka SARI wamewataka kuchoma moto miche ya mahindi ambayo
watagundua imeshambuliwa.
"Wametuambia takriban shamba likishambuliwa, tung'oe mahindi hayo na
kuyachoma moto, wametuambia kama tulishavuna basi tukoboe mahindi hayo maana
kiini chake kina madhara,"alisema.
"Aliongeza kusema" hata tukikoboa mahindi tumeambiwa zile pumba
zake tusiipe mifugo kwa sababu itaathirika... Ugonjwa huu wa mmea wa mahindi
umeleta taharuki kubwa kwa wakulima na wananchi."CHANZO MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment