Sunday, February 1, 2015

On 3:16 AM by Shambani Solutions   No comments
Machungwa ya Tanga
Dodoma. Serikali imesema matunda yanayolimwa katika Mkoa wa Tanga licha ya kuwa ni mengi lakini bado hayana sifa ya kutengeneza juisi.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyetaka kujua ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kiwanda cha matunda Mkoa wa Tanga.
Mbunge huyo alihoji kitendo cha Serikali kubadilisha eneo la kujenga kiwanda na sasa imetangaza kujenga kiwanda hicho eneo la Msoga wilayani Bagomoyo.Mbunge huyo alitaka kuelewa sababu ya Serikali kuwa na kigugumizi cha kujenga kiwanda hicho sehemu yenye matunda mengi kuliko Bagamoyo.
Pia katika swali lake la nyongeza awali, mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutafuta mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kutengeneza juisi ya machungwa mkoani Tanga.
“Wakulima wa Machungwa Tanga hawana soko la machungwa na kusababisha kuoza, je Serikali ina mpango gani wa kumtafuta mwekezaji,” alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alisema machungwa ambayo yanazalishwa mkoani Tanga hayana ubora wa kutengeneza juisi.
Mbali na hilo alisema bado hakuna matunda ya kutosha ambayo yanaweza kukifanya kiwanda kuwa na mwendelezo wa kuzalisha juisi kwani matunda yanayozalishwa Tanga ni ya msimu.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza juisi katika Mkoa wa Bagamoyo na Msoga, Naibu Waziri huyo alisema limetokana na mapendekezo ya mwekezaji mwenyewe aliyependelea eneo hilo zaidi kuliko eneo lenye matunda mengi.

0 comments:

Post a Comment