Saturday, January 17, 2015

On 1:53 AM by Shambani Solutions   2 comments

Habari za leo wapendwa!
Namna tunavyoyaangalia mambo inaathiri sana maisha yetu. Tunavyoangalia mambo ni matokeo ya namna tunavyowaza na kufikiri.
Jambo unaloliwazia vibaya haya siku moja haliwezi kuwa zuri ukiamua kulifanya. Litaishia kuharibika tu na pengine ukalaumu watu wengine kwa kushindwa kwako bila kujua kwamba wewe ndiye mchora ramani wa kushindwa kwako kwa sababu ya kuliwazia vibaya jambo ulilokuwa ukifanya.
Hali hii imewatokea wengi katika masomo, kazi, biashara nk! Kamwe usithubutu katika maisha yako kufanya jambo lolote lile kama unaliwazia vibaya, usilolipenda.
Ukifanya Hivyo nakuhakikishia utaishia kusikitika baadaye, maana asilimia karibu mia ya watu wote hufanikiwa wakifanya mambo wanayoyapenda!

WAZO LA BIASHARA
Leo napenda nizungumzie kuhusu kilimo, kazi ambayo kwa miaka mingi tangu shuleni tulifundishwa kuwa ndiyo UTI WA MGONGO WA UCHUMI WA NCHI YETU. Sina uhakika kauli hii bado ina ukweli ndani yake (maana ukweli wa jana unaweza kuwa uongo wa leo na kinyume chake). Ninachofahamu na ambacho bado ni ukweli ni kwamba; asilimia kubwa ya Watanzania wamategemea kilimo kuendesha maisha yao. Vijana wengi maofisini leo wamesomeshwa kwa kupitia kilimo. Huu ni ukweli.

Lakini kilimo hikihiki kilichotusaidia Watanzania wengi leo hii kinapuuzwa na asilimia kubwa ya watu, hasa vijana. Ni hapa Tanzania kuitwa mkulima ni tusi, siyo sifa! Nimekua nikisikia vijana wakitukana wenzao: "We mkulima nini?" Wapo watu wana ngeo leo walizozipata kwa sababu waliwatukana watu tusi hilo; MKULIMA.

Kwa unyanyapaaji huu wa kilimo, watu wengi, nikiwemo mimi, tulijikuta timekichukia kilimo na kukiona si biashara. Hata tulipotakiwa kufikiria mawazo ya biashara, kilimo hakikuwemo kwenye orodha, tulikiwazia vibaya! Hatukukipenda na tulipojaribu kukifanya tuliishia kutofanikiwa sababu hatukuwa na mapenzi nacho.

Mwaka 2002 nilizinduka katika usingizi mzito wa kutokiona kilimo ni biashara, nikasema “No”! Haiwezekani, kuna siri imejificha katika kilimo. Inawezekanaje! mi' mtoto wa mkulima nidharau kilimo? 


Swali hili lilinifanya niamue kutafuta shamba huko Kiwangwa, Bagamoyo, na kuanzisha kilimo cha mananasi. Naweza kusema kwa sauti ya juu kwamba nilikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kulima mananasi huko Kiwangwa. Hakika nilipata mafanikio makubwa sana katika kilimo cha mananasi. Kwa waliowahi kufika Kiwangwa, watakuwa mashahidi wa jambo hili.
Hapo ndipo nilipothibitisha kwamba; kilimo si ushamba, si tusi, bali kuna siri kubwa sana imefichwa kwenye unyanyapaaji huu wa kilimo. Ndiyo maana leo napaza sauti yangu na kusema; KILIMO NI WAZO LA BIASHARA LINALOWEZA KUMWONDOA KIJANA WA KITANZANIA KWENYE UMASIKINI.

Hili hapa ni angalizo; KAMWE USIJARIBU KUFANYA BIASHARA YA KILIMO KAMA HUKIPENDI! Lazima kwanza uanzishe mapenzi na kilimo kabla ya kuanza biashara hii na uwe tayari kuvumilia. Katika biashara ya kilimo msamiati wa HARAKA, uweke pembeni.
Tafuta zao lolote unalotaka kulima, linaweza kuwa ufuta, mboga, matikiti, mahindi, n.k. Fanya utafiti wako ikiwa ni pamoja na kutafuta ardhi bora. 

Anza kidogokidogo, kisha panua kadri siku zinavyokwenda!
Jambo hili linawezekana, usikubali visingizio. Anza, halafu utaona milango mingine imefunguka! 


Ni kweli Biblia inasema usianze kujenga mnara kabla ya kufanya hesabu kama unaweza kuumaliza! Fungu hili limewafanya Wakristo wengi kubaki walipo wakisubiri kila kitu kitimie ndipo waanze; 
HABARI NJEMA NI KWAMBA ANZA NA ULICHONACHO NA UTAMALIZA NA KILA KITU.

Asanteni,
Ni mimi ndugu yenu,
Eric.

kupata habari hii kamili tembelea link hii: https://www.facebook.com/shigongotz

2 comments:

  1. Asante sana mkuu kwa kutupa uzoefu na kutuhamasisha.Ni kweli kwamba sisi kama viana inabidi tuwe na maono tofauti katika fikra zetu kuhusu kilimo. Binafsi nimehamasika na nimekuwa nikijaribu kufuatiliia na kuona ni namna gani naweza kujihusisha na fikra hizi na hata utendaji katika kilimo.

    ReplyDelete
  2. Asante nimepata kitu kichwani mwangu

    ReplyDelete