Thursday, December 12, 2013

On 4:17 AM by Shambani Solutions   No comments
Muheza. Wakulima wa mkonge nchini wameomba Serikali kuondoa kodi sumbufu ikiwamo ya ardhi, usalama kazini (Osha), kodi ya mafuta, Ongezeko la Thaman (Vat) kwenye nyuzi.

Pia, imetakiwa kuondoa ushuru wa mazao ili kupunguza mzigo wa uendeshaji.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Katibu wa Chama cha Wakulima, Wazalishaji na Wafanyabiashara wa Bidhaa za Mkonge (Sat), Raphael Ngalondwa wakati wa maadhimisho ya siku ya mkonge nchini yaliyofanyika viwanja vya Chuo cha Utafiti Mlingano, wilayani hapa.

Akizungumza mbele ya Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo na Mazao, Beatus Balema aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chistopher Chiza, katibu huyo alisema lengo la kutoa ombi hilo linatokana na mkusanyiko wa kodi nyingi katika sekta ya mkonge.

Ngalondwa alisema kuna haja ya Serikali kuondoa tofauti ya kodi ya kilimo cha mashamba ya mkonge, kati ya maeneo ya vijijini na mijini. Alisema pia wadau wa zao hilo wamekuwa wakilalamikia kodi ya ardhi (Land Rent), ushuru wa mazao (Produce cess) na kodi ya huduma (Industrial Service Levy).

Kuhusu Osha, alisema ni vyema Serikali iangalie upya viwango vinavyotumika ili visiathiri kilimo cha mkonge ambao wakulima wamejitolea kuufufua.

Kwa upande wa kodi ya mafuta, katibu huyo alisema Serikali ingeweza kuiondoa kwa wakulima wa mkonge kwa sababu nchi nyingi duniani wanatumia motisha hiyo. Alisema hata wadau wa mkonge wanalipishwa mardufu kutokana na kulipa kodi ya barabara.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Chiza, Balema aliwapongeza wadau na bodi ya mkonge nchini kwa kuendesha sekta hiyo bila migogoro mikubwa kama ilivyo kwenye korosho, chai, kahawa, pamba na sukari.

Alisema kwa sababu Serikali imeweka utaratibu wa meza ya majadiliano, atafikisha mahala husika maombi kuhusu kodi ili kuweza kufanya mjadala na wadau wa mkonge ili kufikia mwafaka.

Chiza alisema hivi sasa majadiliano ndiyo yanayotawala uendeshaji wa uchumi, hivyo haoni sababu ya kutokufikisha suala hilo.

source:http://www.blogger.com/blogger.g?blogID=6875966675370421464#editor/target=post;postID=1967770535212710676

0 comments:

Post a Comment