Friday, December 27, 2013

On 1:01 PM by Shambani Solutions   No comments

Taarifa ya Uwekezaji Tanzania mwaka 2013 imetaja kuporomoka kwa kilimo huku madini na nishati zikiongezeka kwa kiasi kikubwa.
 
Kwa miaka mingi Tanzania imetaja kilimo kuwa ndiyo uti wa mgongo wa taifa ambapo zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wake hukitegemea, huku ikipanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukikuza, ikiwamo Kilimo Kwanza.

Hata hivyo, taarifa hiyo iliyozinduliwa jana na Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa, jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwavutia zaidi wawekezaji ili kuwekeza katika kilimo nchini.
Pia taarifa hiyo inasema kwamba, mikakati inayoendelea kwenye sekta ya gesi na umeme inahitaji kufuatiliwa zaidi ili kutatua tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.

Pia taarifa hiyo inasema kwamba, mikakati inayoendelea kwenye sekta ya gesi na umeme inahitaji kufuatiliwa zaidi ili kutatua tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dk Natu Mwamba alisema kwamba, utafiti huo  walioufanya Tanzania Bara na Visiwani ulibaini kuwa shughuli za umeme na gesi asilia ambao uwekezaji wake ulikuwa chini ya Dola za Marekani 3 milioni  kati ya mwaka 2008 na 2009 uliongezeka na hadi kufikia Dola 290.5 milioni,  mwaka 2010 na Dola 290.4 milioni mwaka 2011.

Kwa upande wa kilimo, alisema kuwa uwekezaji binafsi ulioingia uliongezeka kutoka Dola za Marekani 21milioni mwaka 2008  hadi kufikia 31 milioni, mwaka 2011.

“Uwekezaji katika sekta ya kilimo uliendelea kuwa mdogo ukilinganisha na sekta nyingine hususan madini na viwanda,” alisema Dk Mwamba aliyekuwa akimwakilisha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu na kuongeza:

“Jitihada za makusudi zinahitajika hasa kuwekeza kwenye miundombinu vijijini, miradi ya umwagiliaji, upatikanaji wa umeme vijijini kwa ajili ya kuwezesha usindikaji wa mazao pamoja na uchoraji wa ramani zenye utambuzi na mgawanyo wa matumizi ya ardhi nchi nzima.”

Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alisema kuwa ili kuongeza sekta ya uwekezaji hasa kilimo ni lazima kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.

Alitaja moja ya mambo yanayokwamisha wawekezaji nchini kuwa ni ufanisi wa bandari za hapa nchini kutokutoa huduma kwa ufanisi kutokana na kuchelewa kutoa mizigo inayoingia nchini.

Dk Nagu alisema suala la wananchi kudai fedha ili kutoa ardhi au jambo lolote la uwekezaji ndani ya eneo lao ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo na kuwafanya wawekezaji kutokuvutiwa kwenda  kuwekeza katika maeneo yao.

Taarifa hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Gesi-na-madini-juu-zaidi--kilimo-kwishnei/-/1597296/2093698/-/gv1jx5/-/index.html

0 comments:

Post a Comment