Saturday, November 30, 2013

On 1:09 AM by Shambani Solutions   No comments
Dr Kingazi alisema maneno hayo alipokuwa anaunga mkono maneno ya ndugu Peter Lanya ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa TCCIA anayeshughulikia kilimo na pia Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Bidhaa nje (Tanzania Exporters Association) amesema kwamba wakulima ni vyema wakaruhusiwa kuuza bidhaa zao mahali ambapo watapata maslahi zaidi.

  
Dr Stephen Kingazi ambaye ni mwanzilishi wa Chama cha wakulima wahitimu cha Tanzania(TGFA ) alisema kuwazuia wakulima kuuza mazao yao soko la nje si kitu chema hata kidogo na wala hakikubaliki.

Alisema kuondolewa kwa ushindani katika kilimo kunasababisha bidhaa kuwa na bei chini na matokeo yake mkulima kuendelea kuwa maskini. Hata hivyo alisema kwamba ipo haja kwa Serikali ya Tanzania kushawishi wananchi kutambua umuhimu wa kuwa na akiba ya chakula.

Dr Kingazi aliendelea kusema kwamba ni vyema kanuni zikawekwa kusaidia kuhakikisha kwamba kuna akiba ya chakula nchini. Aidha Serikali inatakiwa kutambua kwamba ili kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni lazima kuwapatia wakulima mbegu bora. 

“Ukiangalia sasa utaona kwamba mbegu nyingi zilizopo sokoni ni mbaya kuliko zile ambazo wananchi wamezoea kuzitumia, Serikali lazima kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora ili kuongeza tija” alisema Dk Kingazi. Dk Kingazi alishauri Serikali kutumia kila uwezekano kuhakikisha kwamba wakulima wanakwenda sambamba na teknolojia mpya ya kilimo.


Kwa mujibu wa Ndugu Peter Lanya wakulima kazi yao hiyo ndiyo inayowaingizia kipato ambacho zaidi ya asilimia 95 hukitumia kwa ajili ya familia na hivyo kuwanyima nafasi ya kupata kipato kizuri si sahihi.

“Ni jambo la kustaajabisha kuwalazimisha wakulima ambao tegemeo lao la pekee la kuwapatia kipato ni kilimo kuuza bidhaa zao katika soko ambalo halina maslahi kwao. Nadhani ni vyema kuwaacha huru kutafuta masoko yenye maslahi,” alisema Lanya.

Kama wakulima hawataruhusiwa kuuza kwa namna wanayoona wao inafaa, kwa vyovyote watashindwa kuwa na kipato cha kuwasaidia kila siku na kudunduliza fedha zinazotakiwa kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.
“Kama wasipopata fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi ya msingi ya kwao wenyewe kama matibabu hawatakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kilimo kwa msimu unaofuata na hivyo kuongeza kasi ya umaskini,” alisema Lanya.
  
SOURCE:http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Wakulima-wataka-wasibanwe-katika-kutafuta-soko/-/1597592/2091600/-/item/2/-/jg0uf2z/-/index.html

0 comments:

Post a Comment