Wednesday, October 23, 2013

On 3:58 PM by Shambani Solutions   No comments
Raisi wa Tanzania
Njombe. Rais Jakaya Kikwete, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi na watendaji wake, kuangalia namna ya kuruhusu sekta binafsi kununua tani 2,672,902 za mahindi kutoka kwa wakulima Ludewa.Pia ametaka wakulima hao waruhusiwe kuuza mahindi yao nje ya nchi. 

Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Njombe, katika majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo mpya.
“Kuwazuia wakulima kuuza mahindi yao nje ya nchi ni kuwatajirisha wanaokaa kwenye vizuizi na kufanya ulanguzi.
“Ni lazima mkoa uhakikishe kuwa wakulima wanawekewa utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu kuuza mazao yao nje ya nchi,” alisema Rais.
Alisema kufanya hivyo, kutatoa nafasi kwa wakulima, kuinua vipato vyao. Alisema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na ya kuiruhusu sekta binafsi kununua mahindi yaliyopo ili kuondoa uwezekano wa kuwanufaisha wachache.
“Maghala yetu ya akiba ya chakula yana uwezo wa kubeba tani 250,000 kwa hiyo kwa sasa tunatoa fursa kwa sekta binafsi nao watusaidie katika hili maana sisi Serikali tumejaza maghala yetu,” alisema. 

Pia aliwataka viongozi kuendelea kuwahimiza wananchi kulima mazao ya biashara, hasa miti, kahawa, mbogamboga na matunda.

0 comments:

Post a Comment