Sunday, September 15, 2013

On 12:22 PM by Shambani Solutions   No comments
Kibibi Muhogo
Ukipita katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Unguja, Kibibi Mihogo ni miongoni mwa majina maarufu.Umaarufu wa jina hilo umetokana na mchango wake katika kufanikisha mambo mbalimbali kwenye jamii hasa kwa wanawake wa Zanzibar, akielemea zaidi katika masuala ya kilimo, utafiti na harakati za kupunguza umaskini. 
Kibibi Mihogo ambaye jina lake halisi ni Kibibi Mwinyi Hassan ni mzaliwa wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini, Unguja katika Visiwa vya Zanzibar.Ni mtoto wa kwanza kati ya wanne kwa baba mmoja na mama mmoja, akiwa na ndugu wengine wa baba mmoja mzee Mwinyi Hassan. Mwanamke huyu ambaye pia ana watoto wanne akiwa pia ni mjane baada ya mumewe kufariki dunia, Juni mwaka jana, alianza safari yake ya elimu katika shule ya msingi iliyopo kati ya Kijiji cha Bwejuu na Paje. Baadaye alijiunga na Sekondari ya Machipi iliyopo Ifakara, wilayani Kilombero, Morogoro, ambapo alisoma mchepuo wa kilimo na kuhitimu mwaka 1979.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, wilayani Kilindi mkoani Tanga, alipokuwa kikazi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba anayoifanyia kazi sasa, Kibibi aliye na Shahada ya Uzamili ya Rasilimali Watu, anaeleza kuwa baada ya kumaliza kidato cha nne alijiunga na Chuo cha Kilimo Ilonga, wilayani Kilosa, pia mkoani Morogoro kabla ya kuajiriwa na Wizara ya Kilimo Zanzibar katika Idara ya Elimu kwa Wakulima. “Kati ya mwaka 1982 hadi 1985 nilifanya kazi ya vipindi vya kilimo katika Televisheni ya Zanzibar (TVZ) na vipindi vya redio, Sauti ya Tanzania Zanzibar. Pia nilikuwa nikitoa ushauri kwa wakulima. Mwaka 1986 nikaenda kusomea Diploma ya Kilimo na Uzalishaji Mazao, nikahitimu mwaka 1988,” anaeleza Kibibi. Anasema kuwa baada ya hapo alipangiwa kazi katika Kituo cha Utafitijeni wa Mazao ya Mizizi maarufu Kizimbani mjini Zanzibar na kuwa Ofisa Utafiti wa zao la muhogo na nazi.“Utafiti ulinifundisha mengi, nilisafiri nchi nyingi, ulinifanya nijulikane Unguja yote. Nilikutana na wakulima, pia kuwafundsha uandaaji na uzalishaji mazao bora ya mizizi hasa mihogo, niliojifunza Nigeria. Niliweza kutambua aina ya mihogo na magonjwa ya mimea kwa kutazama majani yake tu na hapo ndipo nikapewa jina la Kibibi Mihogo. Najivunia utaalamu na kujulikana ,” anasimulia.
Kibibi anamtaja Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin Amour Juma kuwa alimwezesha kupata shahada baada ya kuwatangazia Wazanzibari nafasi za udhamini wa masomo nchini Mauritius mwaka 1998, ambapo miaka mitatu baadaye alihitimu na aliporejea Zanzibar alikuwa mkuu wa Maabara ya Kuzalisha Mbegu katika Kituo cha Utafiti Kizimbani.Hata hivyo anasema: “Moyo wangu ulichoka, nilipenda mazao ya mizizi, nilipenda kukutana na wakulima, sikupenda kazi ya maabara; …sikufanikiwa. Nilitaka kwenda katika siasa, nikaacha baada ya kuona aina ubaguzi hasa kwa watu wapya kwenye siasa, nikakata tamaa.”

Anabainisha kuwa wakati wote akifanya kazi Wizara ya Kilimo, alijihusisha na shughuli mbalimbali hasa kwa wanawake ikiwamo uanzishaji wa vikundi vya maendeleo, ambapo baadaye alihamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais.
“Napenda kujali wanawake wa hali ya chini, niliwahi kuanzisha kikundi cha wanawake 70 nikawa mwenyekiti wa biashara ndogondogo tulifadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Kusaidia Wanawake iitwayo Woman Enterprises Development Trust Fund (WEDTF), waliotoa mikopo. Nilisimamia urejeshwaji. Umoja huo unaendelea:
Tukaanzisha Magomeni Saccos (Zanzibar) nikiwa mwenyekiti, sasa tuna wanachama 350,” anaeleza Kibibi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba.Anaeleza kuwa katika utendaji wake kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aliwahi pia kuwa mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) akiwa chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, wakati huo Amina Salim Ali.
Kibibi anasema kuwa akiwa Mratibu wa Saccos, alikutana na wananwake wengi pia vikundi tofauti vya kijamii vinavyopigania maendeleo na kuwawezesha kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wanawake na watoto. Anabainisha: “Kazini sikujali muda wa kutoka bali kuwahi kuingia ofisini, nilijituma. Niliwaongoza wanawake kuanzisha miradi hasa ya kilimo na biashara kwani ndiyo mkombozi. Niliwashauri pia kwenda shule kuongeza maarifa. Hiyo ndiyo siri yangu hata kufika nilipo sasa.”
Anasema kuwa alihamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo baada ya kuonekana anaweza alibahatika kuingia katika vikao mbalimbali vya Serikali na kuandika ripoti za vikao tofauti, kutoka hapo aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kupendekezwa na Taasisi ya WEDTF, kazi anayoendelea nayo hadi sasa.
“Matajarajio yangu ni Tanzania kupata Katiba nzuri yenye masilahi kwa pande zote za Muungano ambazo ni Zanzibar na Tanzania Bara,” anasema na kuhitimisha: “Wito wangu, wanawake wasiwe nyuma, wasiwe tegemezi, wasikate tamaa, waongeze elimu. Wahimize pia watoto kwenda shule kupata elimu na siyo nyumba au mali nyingine ambazo wakiwa na elimu watazipata tu. Kwangu binafsi kubwa ni wanangu wasome hata zaidi yangu, naomba Mungu anifanikishe hilo.”

0 comments:

Post a Comment