Friday, September 27, 2013

On 12:11 AM by Shambani Solutions   No comments
Mbegu dhaifu zinahitaji uangalizi wa hali ya juu kwa sababu mkulima asipokuwa makini, zitazaa matunda yasiyo bora.
Wakulima wengi nchini wamekuwa na mazoea ya kutayarisha mashamba yao bila kufuata msingi sahihi inayozingatia kilimo bora na kusababisha wakulima hao kupata hasara.Mara nyingi hali hiyo inatokana na wakulima kutokuzingatia ushauri wa kitaalamu, kwa mfano, kilimo bora chenye tija.
Mbali na hayo ili kujua changamoto zinazoikabili sekta ya pamba kupitia kilimo cha mkataba sambamba na umuhimu wa Mfuko wa Maendeleo ya Pamba  (CDTF), Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Gabriel Mwallo na Meneja wa CDTF, Essau Mwalukasa, wanazungumzia mambo mbalimbali yanayohusu kilimo hicho cha mkataba. Mwalukasa anasema kazi ya mfuko huo unaojumuisha wakulima, wafanyabiashara na Serikali ni kununua pembejeo za kilimo kutoka nje kwa manufaa ya wakulima.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wakulima kupitia kilimo cha mkataba,  Mwallo anasema kilimo cha mkataba kinawasaidia wakulima kupata dawa za mimea na mbolea, mazao bora kutokana mbegu bora wanazopewa wakulima.Mwallo anaeleza kwamba mbegu dhaifu inahitaji uaangalizi wa hali ya juu kwani inazaa matunda yasiyo na ubora. “Gharama za utunzaji wa mbegu dhaifu ni kubwa kwa kuwa mkulima atalazimika kununua dawa nyingi ili kupata mbegu bora,” anasema.
Ameongeza kuwa iwapo mmea dhaifu utakosa dawa hizo mara kwa mara pamba itakayotoka itakuwa na weupe hafifu. Anasema kutokana na kuwapo wa dawa zenye kiwango cha chini, itamlazimu mkulima kuingia gharama zaidi kununua dawa.Kaimu Mkurugenzi huyo wa TCB, anasema ili kupata mmea bora wataalamu wanashauri mkulima kupanda kiasi cha mbegu takribani 22,200 kwa ekari moja.  “Kwa mbegu bora mkulima anaweza kurudia mara mbili kuweka dawa ya kuzuia wadudu, lakini kwa mbegu dhaifu itamlazimu mkulima kurudia mara kwa mara kwa kiwango cha  asilimia 85,” anasema.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa mvua, Mwallo anasema: “Kilimo chetu nchini Tanzania kinategemea mvua kwa asilimia 100, lakini kwa bahati nzuri zao la pamba ni kati ya mazao yanayohimili ukame.”Mwallo anasema CDTF imelenga kusimamia maendeleo ya pamba sambamba na kuitangaza kwa ushirikiano na TCB na Kampuni ya Usambazaji wa Pembejeo nchini (MUKPAR).
Kabla ya mfuko wa CDTF, TCB ndiyo iliyokuwa na jukumu lote la kusimamia na kuendeleza sekta ya pamba katika suala zima la kulima, masoko na utangazaji. Lakini baada ya mabadiliko ya sheria,TCB ilipewa jukumu la kusimamia maendeleo ya sekta hiyo ya pamba.“Baada ya Serikali kuanzisha sera ya ubinafsishaji wadau kutoka sekta binafsi walitakiwa kushiriki katika kuendeleza sekta ya pamba nchini. Sasa kutokana na hili ikazaliwa CDTF ambayo inaundwa na wakulima wa pamba,” anasema Mwallo.
Akizungumzia dawa ya Bamesrini, Mwallo anasema dawa hiyo ililalamikiwa na kufanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Uchunguzi wa Mbegu za Kilimo (PPRI)na kugundua kuwa haikuwa na tatizo. “Haikuwa na tatizo isipokuwa ilikuwa na ujazo wake ulikuwa ml120 badala ya ml160. Hii ilisababisha matatizo wakati mkulima akichanganya dawa hiyo na maji ambapo maji yanakuwa mengi zaidi kuliko inavyotakiwa,” anasema.
Kaimu Mkurugenzi wa TCB anaeleza changamoto nyingine wanazokumbana nazo kuwa ni baadhi ya wakulima kuchanganya pamba na mchanga ili kuongeza uzito. Akielezea namna nzuri ya kuweza kurekebisha upungufu uliyopo kwenye mfuko huo, Mwalukasa amesema mfumo mzuri unapaswa kuwapo wa kusambaza pembejeo kwa wakulima. “Ingekuwa vyema wadau wakae pamoja na kupata mfumo mzuri wa kuendesha mfumo huu. Ninaamini kwa pamoja tunaweza kupata suluhisho zuri,” anasema.

0 comments:

Post a Comment