Friday, March 1, 2013

On 3:04 PM by Shambani Solutions   No comments


Msanii wa bongofleva LINEX
NI Mkulima aliyetua jijini Dar es Salaam miaka kumi iliyopita, akitokea Kasulu, mkoani Kigoma. Huyo si mwingine bali ni Sande Mangu, maarufu kama Linex aliyekuja Dar kwa lengo moja tu, la kutafuta mwanya wa kutokea katika sanaa ya muziki wa Bongo Fleva.

Linex ni mtoto wa kwanza katika familia yenye vipaji  vya uimbaji. Katika ulimwengu wa muziki msanii huyo alijitambulisha na kibao cha ’Halima’, baadaye akatamba na vibao kama Aifora na Bodaboda. Hata hivyo sasa ameibuka na kibao kipya kiitwacho, Mahakama ya Mapenzi.  Thamani ya jina la msanii huyu iliongezeka kwa kasi, baada ya kutoka na wimbo wa ’Lekatutigite’ akiwa na kundi la 255 lililoundwa na wasanii kutoka Mkoa wa Kigoma, baadhi wakiwa ni Diamond, Chegge, Queen Darlin, Ali Kiba, Mwasiti na Ommy Dimpoz.

Kazi za kilimo
Mbali na muziki, Linex mkulima wa zao la vitunguu swaumu vinavyomsaidia kujiongezea kipato. “Mimi ni mkulima mzuri tu wa vitunguu swaumu kule nyumbani Kasulu. Nilikwama kidogo kuendelea kutokana na kazi za muziki, ila kwa sasa nina mpango wa kuwekeza zaidi katika kilimo hicho kwa kuwa kilikuwa kikiniingizia pesa nzuri,”anasema Linex.

Anabainisha sababu za kujitosa katika harakati za kilimo kuwa ni mipango yake binafsi ya kujiongezea kipato cha uhakika badala ya kutegemea kazi ya muziki pekee.
Nyuma ya pazia

Uwezo alionao Linex katika sanaa ya muziki unatokana na asili yake. Kwa maneno yake, anabainisha kuwa kwa asili ukoo wa mama yake ni waimbaji. “Kuanzia babu, mama zangu wadogo na dada zangu wote wanaimba na kwa sasa ni wake za wachungaji. Bado wengine wanaimba kwaya makanisani, kwa hiyo utaona nimetokea katika mazingira gani,”anafafanua. Pamoja na umaarufu ambao umekuwa ukiwalewesha wasanii wengi, Linex ameendelea kuwa karibu na familia yake. “Mimi familia yangu ndiyo kila kitu, hata kama nitafanikiwa kwa kiwango gani, bado haiwezi kunibadilisha. Familia iko poa na maisha yanakwenda,”anaeleza Linex.

Kuhusu uhusiano anadokeza kuwa ameamua kuwa mwaminifu mbele ya kimwana mmoja wa Kibongo, ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina. Linex anabainisha kuwa katika maisha yake starehe yake kubwa ni kuimba wakati wote akisema: ”Ninapoimba, mie ndiyo starehe yangu. Kwa kweli sina tabia ya umalaya au ulevi.”

Msanii huyo, ambaye kwa sasa anatamba na kibao cha Mahakama ya Penzi, anaweka wazi kuwa kwa sasa hatakuwa tayari kufanya kazi za kishkaji kutokana na makosa yaliyojitokeza kwa mwaka uliopita. “Yaani zile kazi za kishkaji sitafanya tena kwa sababu nimegundua hazitanisadia, badala yake zitanifanya kuwa maskini daima. Bora lawama, kuliko hasara,”anasema Linex. Mbali na hilo anabainisha kuwa thamani yake kwa sasa siyo kama ilivyokuwa ikifikiriwa na wadau wengi wa muziki na kwamba hatakuwa tayari kufanya kazi katika ukumbi usiokuwa na watu zaidi ya 500.
 
Mbali na kutoamini zaidi ukuaji wa muziki kupitia wasanii wa nje, Linex anaweka wazi kuwa kwa sasa ana mpango wa kufanya ‘colabo’ na Keko, ambaye ni rapa maarufu kutoka nchini Uganda.
“Siyo hivyo tu, bali kuna mipango mingi sana, yaani nahitaji kuzingatia muda wangu zaidi, ili kuifanikisha. Kuna  wasanii kama Bebe Cool na Zahara wa Afrika Kusini, wote hawa wako kwenye ratiba yangu ya kufanya nao kazi,”anadokeza Linex. Bofya apa ili uendelee kusoma habari hii

0 comments:

Post a Comment