Friday, January 25, 2013

On 1:08 PM by Shambani Solutions   No comments



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA
  
 
TAARIFA KWA UMMA  KUHUSU BEI ZA VYAKULA MIKOANI


UTANGULIZI: 

Tulianza msimu huu 2012/13 tukiwa na ziada kidogo ya chakula na kwa kujitosheleza kwa asilimia 113. Msimu huu, tofauti na msimu uliopita hatukuzuia wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi.

Pamoja na uzalishaji tuliokuwa nao katika maeneo kadhaa ya nchi kulikuwepo na maeneo ambayo uzalishaji wake haukuwa wa kuridhisha kutokana na hali mbaya ya hewa na hivyo kuwa na upungufu wa chakula.  Upungufu huu unajidhihirisha kutokana na kupungua  kwa uingiaji na upatikanaji wa vyakula sokoni, hususan unga wa mahindi ambacho ni chakula kikuu    na  bei ya soko kupanda  sana kwa viwango vilivyo juu ya bei ya wastani nchini.

Uchambuzi wa bei za vyakula unaonesha kwamba bei ya wastani ya mahindi kitaifa ni shilingi 675 kwa kilo.  Aidha, bei ya mahindi katika masoko ya miji mkuu ya baadhi ya mikoa iko juu ya wastani.  Kwa mfano, bei ya Dar es Salaam tarehe 28 Novemba, 2012 ilifikia shilingi 750 kwa kilo, Mwanza shilingi 825, Moshi shilingi 700, Tanga shilingi 785, Tabora shilingi 750 na Mtwara shilingi 735.  Aidha, unga wa sembe uliuzwa kati ya shilingi 1,100 na shilingi 1,500 kwa kilo, mwezi Desemba 2012.

Hali ilivyo katika maeneo mengi ya nchi ni kwamba, viwango vya upatikanaji wa chakula vinatofautiana katika maeneo mbali mbali.  Wakati mikoa minane (8) ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro ilikuwa na ziada ya chakula, mikoa saba (7) ya Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida na Dodoma ilikuwa na hali ya utoshelevu tu na mikoa sita (6) ya Shinyanga, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dar es Salaam ilikuwa na uhaba wa chakula.

Kutokana na upungufu wa chakula kuzidi kujitokeza, mwezi Oktoba, 2012, Serikali, kupitia Kamati ya Maafa iliidhinisha mgao wa tani 18,417.8 wa chakula cha njaa kutoka katika maghala ya Hifadhi ya Chakula ya Taifa (National Food Reserve Agency) kwenda katika Halmashauri 35 za mikoa 12 zilizobainika kuwa na upungufu mkubwa wa chakula.  Mikoa iliyopewa chakula cha njaa ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

Kutokana na hali ya upungufu wa chakula kuzidi kuendelea na kujitokeza kwa majanga mengine kama mafuriko, Serikali iliidhinisha mgao wa nyongeza ya chakula hadi kufikia tani 26,958.300 kwa Halmashauri zilizokuwa  na mahitaji makubwa ya chakula cha msaada.  Aidha, upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo yanayozalisha nafaka kwa wingi umesababisha kupungua kwa chakula kinachosambazwa katika soko hivyo kufanya usambazaji wa chakula kutolingana na mahitaji ya soko. Hali hii imesababisha kupanda kwa bei ya mahindi na unga wa  mahindi katika baadhi ya masoko hususan  ya mijini. Ili kukabiliana na hali hiyo Serikali imechukua  hatua zifuatazo:-
(i)      Kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yaliyokuwa na upungufu wa chakula.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye upungufu wa chakula Serikali iliendelea kuongeza mgao wa chakula cha msaada kutoka tani 18,417.8 hadi kufikia  tani 28,250.300. Hadi kufikia mwezi Januari, 2013 jumla ya tani 19,040.865 za mahindi zilishachukuliwa. Aidha, jumla ya tani 9,209.435 bado hazijachukuliwa na mikoa iliiyopewa mgao wa nyongeza. Mikoa ambayo bado haijachukua nyongeza hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Mbeya na Mara. Kiambatisho Na. 1
(ii)    Kuuza tani 40,000 za mahindi kutoka kwenye ghala la Taifa kwa ajili ya kushusha bei ya unga wa mahindi.

Serikali imeidhinisha kuuzwa tani 40,000 za mahindi kutoka katika ghala la chakula la taifa ambapo tani 20,000 zitauzwa kati ya mwezi Januari na Februari, 2013. Kwa bei ya shilingi 450 tu kwa kilo. Kiasi kingine cha tani 20,000 kilichobaki kitauzwa kuanzia mwezi Machi katika maeneo yatakayobainika kuwa na upungufu wa chakula na bei kuendelea kupanda. Mgao Kimkoa ni kama inavyoonyesha kwenye Kiambatisho Na. 2.

2.        UTARATIBU WA KUUZA MAHINDI KWA WASAGISHAJI
Mikoa yenye bei ya mahindi iliyo juu ya bei ya wastani kitaifa ndiyo iliyopewa mgao. Mikoa hiyo na mgao wake katika mabano ni kama ifuatavyo:  Arusha (tani 1100), Dodoma (tani 400), Kilimanjaro (tani 400), Lindi (tani 400), Mara (tani 900) , Manyara (tani 800), Morogoro (tani 400), Mwanza (tani 2500), Shinyanga (tani 1029), Singida (tani 500), Tabora (tani 1000), Tanga (tani 700), Mtwara (tani 600) , Pwani (tani 700), Simiyu (tani 1971) na Dar es Salaam (tani 6400).
Utaratibu unaotumika kuuza mahindi kwa wasagishaji ni kama ifuatavyo:
  i.        Mikoa imeelekezwa kuteua wasagishaji waaminifu wenye nia na uwezo wa kusagisha unga kwa ajili ya kuuza kwa walaji kwa bei elekezi iliyopangwa na mkoa ambayo ni kati ya shilingi 750 hadi 900 kwa kuzingatia gharama za usafirishaji.
 ii.        Wasagishaji walioteuliwa wanatakiwa kukidhi vigezo vilivyowekwa kama vile, uwezo wa kulipa fedha za mahindi ndani ya muda uliopangwa, uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mahindi anachonunua, uwezo wa kusagisha, kufungasha na kusambaza unga ndani ya siku saba kuanzia siku aliyochukua mahindi, pamoja na kukubali kuuza kwa bei elekezi.
iii.        Wasagishaji walioteuliwa na mikoa watapewa vibali na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ili waweze kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala kama watakavyopangiwa.
iv.        Mikoa itaingia mikataba na wasagishaji walioteuliwa na kusimamia utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta manufaa yaliyokusudiwa.


v.        Mikoa itachukua hatua kwa msagishaji ambaye atabainika kutumia vibaya kibali alichopewa, kama vile kuuza kibali hicho kwa msagishaji mwingine, kusafirisha na kuuza mahindi au unga kwenye maeneo tofauti na aliyopangiwa, kutosagisha na kuuza unga ndani ya siku saba kwa mujibu wa mkataba.
3.   UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUPUNGUZA BEI YA UNGA KWA WALAJI
Mikoa iliyopewa mgao imeelekezwa utaratibu wa kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hadi kufikia tarehe 14 Januari, 2013 jumla ya mikoa 11 kati ya Mikoa 16 ilikuwa imewaslisha orodha ya wasagishaji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Mikoa hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani,Tanga na Dar es Salaam. Mikoa ambayo haijawasilisha orodha ya wasagishaji ni Mwanza, Tabora, Shinyanga, Mara. 

Kuendelea kuchelewa kuwasilisha orodha ya wasagishaji kunasababisha kuchelewesha zoezi zima la utoaji wa mahindi, usafirishaji, usagishaji na hivyo kuchelewesha unga kuingia sokoni hali inayosababisha bei kuendelea kupanda.  Mikoa hiyo inaagizwa kuwasilisha orodha ya wasagishaji ndani ya siku saba kuanzia sasa.  Jumla ya wasagishaji 127 tayari wameshapewa vibali vya kununua mahindi yanayofikia tani 12,520.00 ambapo tani 7,858.291 zimeshalipiwa na uchukuaji unaendelea lakini kasi ya kulipia na kuchukua ni ndogo. Orodha ya Wasagishaji kama ilivyowasilishwa na mikoa na kiasi walichoidhinishiwa kununua imeoneshwa katika Kiambatisho Na.3.

Serikali inawaagiza Wasagishaji wote waliopewa vibali vya kununulia mahindi kuhakikisha wanalipia na kuchukua kiasi chote cha mahindi kama walivyoidhinishiwa katika vibali vyao ndani ya siku saba kuanzia sasa, vinginevyo Serikali italazimika kufuta vibali hivyo na kuvigawa upya kwa Wasagishaji wengine katika mikoa husika wenye nia thabiti ya kufikisha unga sokoni.
4.  USIMAMIZI NA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI
Wakuu wa Mikoa  na Wilaya wanaagizwa kusimamia na kufuatilia kikamilifu utekelezaji wa zoezi hili kama ilivyoelekezwa. Aidha, mikoa inatakiwa kuweka mfumo mzuri wa usimamizi na usambazaji wa unga unaotokana na mahindi yaliyonunuliwa kutoka katika ghala la Serikali ikiwa ni pamoja na kuwafahamisha wananchi maeneo ambayo unga huo unapatikana pamoja na bei elekezi iliyopangwa na mikoa.
Katika ngazi ya Taifa Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa mkakati huu katika mikoa yote iliyopata mgao wa chakula cha njaa au mgao ulitolewa kwa wasagishaji kwa ajili ya kupunguza bei ya unga katika masoko ya mijini.
5. MWISHO
Kwa kuwa maghala ya Dar es Salaam (Kipawa), Arusha, Dodoma na Shinyanga yana upungufu wa akiba ya chakula kulinganisha na mahitaji ya sasa katika maeneo hayo,  Serikali inaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yenye akiba ya kutosha kwenda katika maghala yenye upungufu ili kurahisisha usambazaji wa chakula katika maeneo yenye upungufu. Tunaendesha zoezi hili la kuhamisha  chakula kwa kutumia Shirika la Reli (TRL) , Jeshi la Wananchi na wasafirishaji binafsi ili kuhakikisha kwamba chakula kinafika haraka.

0 comments:

Post a Comment